Monday, May 23, 2011

Ancelotti atimuliwa umeneja wa Chelsea

Carlo Ancelotti
Carlo Ancelotti
Chelsea imemtimua meneja wake Carlo Ancelotti baada ya kumaliza msimu wake wa pili bila kombe lolote.
Alitimuliwa baada ya Chelsea kumaliza Ligi msimu huu kwa
kuchapwa bao 1-0 na Everton na klabu hiyo ikimaliza kwa kushika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya England.
Ancelotti mwenye umri wa miaka 51 mkataba wake ulikuwa umalizike mwakani katika klabu ya Chelsea.
Taarifa ya klabu hiyo imesema: "Matumaini yetu kwa msimu huu yamekuwa mabaya kutokana na matokeo tuliyopata tofauti na tulivyotarajia na klabu inaona ni sawa kabisa kufanya mabadiliko haya kwa ajili ya maandalizi mazuri ya msimu ujao."
Wameshindwa kubeba kombe la Ubingwa wa Ligi na kuikodolea macho Manchester United ikichukua kombe hilo kwa mara ya 19 wiki moja iliyopita, pia Chelsea wakatolewa katika mbio za kuwania Ubingwa wa Vilabu kwa nchi za Ulaya, wakatupwa nje kombe la FA na vilevile kuwania Kombe la Carling msimu huu.
Chelsea ambao walikuwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu na Kombe la FA msimu huu uliopita, wamemaliza pointi tisa nyuma ya Manchester United na wamewatangulia Manchester City walioshika nafasi ya tatu kwa tofauti ya mabao tu.
Meneja wa zamani wa klabu hiyo Avram Grant naye alikumbana na hali kama hiyo wakati Chelsea ilipomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya England na ikashindwa katika fainali ya Ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 kwa mikwaju ya penalti.
Na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich, aliyemsajili Fernando Torres kwa kitita cha paundi milioni 50 wakati wa usajili mdogo mwezi wa Januari, sasa ataanza hekaheka za kumpata meneja mwengine mwenye uwezo wa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kutoka kwa Manchester United na pia tamaa kubwa ya klabu hiyo ya kubeba kombe la klabu bingwa ya Ulaya.

No comments:

Post a Comment