POLITICS.

Wabunge CCM wamtaka Rais Kikwete Dodoma  
Friday, 05 August 2011 08:31
Rais Jakaya Kikwete ambaye wabunge wa chama chake wamemtaka Bungeni ili kujibu hoja ya wabunge wanaolala Bungeni
WASEMA WAMECHOSHWA NA MAWAZIRI ‘ WANAOLALA’ ,PINDA ANUSURU BAJETI YA UCHUKUZI
Mussa Juma, Dodoma
BAADA ya kuitoa jasho Serikali katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, wabunge wa CCM sasa wanataka kukutana haraka iwezekavyo na Rais Jakaya Kikwete ili waweze kuweka wazi jinsi walivyopoteza imani na baadhi ya mawaziri na watendaji wengine serikalini.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha kamati ya wabunge wa CCM ambacho kilifanyika jana mchana, wabunge hao walieleza wazi kutoridhishwa na utendaji wa Serikali.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine kililenga kuwabembeleza wabunge wa CCM kupitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mmoja wa wabunge hao aliliambia Mwananchi kuwa wabunge waliozungumza walionesha kupoteza imani na baadhi ya watendaji wa Serikali hasa mawaziri ambao baadhi “wamekuwa wakilala bungeni”.

Kwa mujibu wa habari hizo, mbunge wa Longido, Lekule Lazier ndiye aliibuka hoja ya kumuomba Waziri Mkuu, kumweleza Rais Kikwete kuwa wanamuomba afike Dodoma wazungumze kwa maelezo kwamba mambo sio shwari kwa wasaidizi wake.

Hoja hiyo ya Lekule iliongezwa nguvu na hoja la Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alionyesha wasiwasi kuhusu uadilifu wa baadhi ya watendaji serikalini, kutokana na tabia yao ya kuvujisha siri za Serikali kwa wabunge wa upinzani.

Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa wabunge hao, waliombwa kusaidia Serikali kupitisha bajeti hiyo kwani kutofanya hivyo ni kuwaongezea nguvu wapinzani bungeni.

Wabunge ambao walizungumzia hoja hiyo ni pamoja na mbunge mkongwe, Anna Abdalah, ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa CCM ndani na nje ya Bunge.

Abdalah pamoja na wabunge wengine, waliwasihi wabunge wenzao hasa vijana kuwa wavumilivu kwa Serikali ya CCM ambayo inajitahidi kufanya kazi kubwa ya kusaidia, lakini ukata bado ni tatizo.

Habari toka katika kikao hicho, zinaeleza jitihada za Naibu Waziri wa Ajira na Kazi, Makongoro Mahanga kutaka kumtetea, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi kuhusiana na tuhuma za kuuza kinyemela Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) katika kikao hicho zilikwama.

“Mheshimiwa Makongoro, aliinuka na kuzungumza kamtetea Dk Masubiri bila mafanikio,”alieleza mtoa habari huyo.

Kikao hicho cha wabunge wa CCM, kilitanguliwa na kikao kingine cha juzi usiku cha baadhi ya wabunge wa CCM ambao walichangia bajeti na kusisitiza kuwa hawataipisha.

Mmoja wa wabunge hao wa CCM alifafanua kuwa, walishangazwa kuitwa kwa Waziri Mkuu, muda mfupi baada ya Bunge kuahirishwa na kuahidiwa kuwa Serikali itatoa fedha zaidi kwa bajeti hiyo.

“Sasa kama kulikuwa na fedha zaidi ni kwanini walituletea bajeti ndogo kiasi kile na hizo Sh95 bilioni zilipatikana wapi harakaharaka…hili tunadhani ni tatizo la watendaji wetu wa serikali,”alisema Mbunge huyo.

Alisema kwa mazingira hayo, wamebaini kuwepo kwa upungufu mwingi katika utendaji wa Serikali na kwamba hali hiyo inatokana na uzembe wa baadhi ya mawaziri na watendaji wengine.

“Sasa wametuomba tupitishe hii bajeti sisi kama wabunge wa CCM tumekubali, lakini kwa kutoa angalizo kuwa lazima sasa watendaji wa Serikali wafanye kazi kwa uadilifu na kutokiangamiza chama,”alisema Mbunge huyo.

Bajeti yapita
Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ilipitishwa jana baada ya kuwepo mjadala mkali huku wabunge wa CCM na wale wa upinzani bila kujali itikadi zao kutamka wazi kuwa hawaungi mkono bajeti hiyo.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu aliwachekesha wabunge wakati akihitimisha hoja hiyo alipotamka kwa sauti "Mheshimiwa Spika" mathalani ya ile inayotolewa na mpambe wa Bunge pindi vinapoanza au kufungwa vikao vya Bunge.

Alipoona wamecheka sana akarudia ''Mheshimiwa mwenyekiti", wakacheka zaidi na ndipo alipohitimisha hoja yake kwa kutamka vyema kwa kuanza na "Mheshimiwa Spika''

Awali akiwasilisha bajeti hiyo aliliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Sh 237.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji  wa miradi na mipango mbalimbali ya wizara hiyo.

Pinda amwokoa Nundu
Mapema jana asubuhi, Pinda aliwasilisha taarifa ya Serikali ya kuongezea wizara hiyo kiasi cha Sh95 bilioni ili iweze kuendeleza miradi ya Reli ya Kati, kufufua shirika la Taifa la Ndege (ATCL) na ununuzi wa Meli.

Pinda alitoa taarifa hiyo ya Serikali jana , baada ya Spika Anne Makinda kutoa ufafanuzi kuwa, Waziri Mkuu anaweza kutumia kipindi cha maswali na majibu kutoa taarifa ya Serikali kwa dakika zisizozidi 15 na baadaye kipindi cha maswali kuendelea.

Akisoma taarifa hiyo, Waziri Mkuu  alisema  baada ya kusikiliza maoni ya wabunge,  juzi jioni Serikali ilikutana na kuona kuna haja ya kuoingezea fedha wizara hiyo.

“Yaliyojitokeza yalionesha uzito..michango ilikuwa ni mizuri na ninawashukuru,  Rais Kikwete aliamua kuunda wizara hii pamoja na wizara ya ujenzi kutoka wizara ya miundombinu kutokana na uzito wa wizara hizi,”alisema.

Alisema sekta ya uchukuzi inahitaji mitaji mikubwa ili kufanikisha miradi ya Reli, Ndege na mingineyo hivyo ina mahitaji  makubwa, lakini pia bajeti haitoshelezi.

“Jana Serikali ilikutana kutazama uwezekano wa kuongeza bajeti.. sasa tumeridhia na tumekubali  zitaongezewa Sh95 bilioni ambazo zinaweza kutumika katika kusaidia Reli ya Kati, ATCL na ununuzi wa Meli katika maziwa Tanganyika, Nyasa na Ziwa Victoria,”alisema Pinda.

Juzi idadi kubwa ya wabunge, walitamka wazi kuwa kama wizara hiyo, isipoongezewa fedha hawatapitisha bajeti hiyo, huku wakitaka Reli ya Kati na ATCL kupewa kipaumbele.

Vigogo wa UDA kuchunguzwa
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imewaagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (Takukuru) kuanza uchunguzi juu ya kuuzwa kwa UDA.

Pinda alisema uchunguzi huo utafanyika sambamba  na ule utakaofanywa na Kamati Ndogo ya Bunge ya Miundombinu na kwamba Serikali itatoa ushirikiano ili kazi hiyo iweze kukamilika haraka.

“Baada ya uchunguzi kukamilika Serikali itachukuwa hatua za kisheria kwa wahusika wote,”alisema Pinda.

Juzi wabunge walishauri kukamatwa mara moja kwa watuhumiwa wote sakata hilo wakiwamo, Meya wa Jiji, Dk Didas Masaburi, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya UDA, Idd Simba na Mbunge wa Urambo Magharibi, Juma Kapuya kwa madai kwamba ni wahusika wakuu wa kuuza mali za shirika hilo kwa Kampuni ya Simon Group Ltd ambayo inaaminika mwanahisa mmoja wao ni mtoto wa kigogo nchini.