Wednesday, May 25, 2011

`Nec ilichangia kuvuruga Uchaguzi Mkuu mwaka jana`

NA RICHARD MAKORE

Chapa
Maoni
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa
Kila kinapofika kipindi cha Uchaguzi Mkuu hapa nchini huwa kunaibuka mambo mengi ambayo yanahusisha wanasiasa na vyama vyao.
Wanasiasa huwa wanajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha wanaungwa mkono na wapiga kura wao huku vyama navyo vikipiga debe ili kuhakikisha vinaibuka washindi kwa kupata Wabunge wengi, Madiwani ama Rais na hatimaye kuunda serikali.
Mwaka jana ulikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa mara ya nne ambao ulihusisha vyama vingi tangu mfumo huo ulipoanzishwa hapa nchini mwaka 1992 ambapo vyama 18 vyenye usajili vilishiriki katika ngazi mbalimbali.
Kuna baadhi ya vyama vilisimamisha wagombea wa Urais, Ubunge na Udiwani na vipo vilivyosimamisha baadhi ya majimbo ama Kata lakini nafasi ya urais havikusimamisha mgombea.
Wiki iliyopita Vyama hivyo vya siasa na baadhi ya waliokuwa wagombea kupitia vyama hivyo walikutana ili kujadili majeraha ya Uchaguzi Mkuu uliopita ambao ulifanyika mwezi Oktoba 2010.
Katika mjadala huo, vyama hivyo vya siasa pamoja na waliokuwa wagombea wao na ambao hawakugombea nafasi yoyote mwaka jana kwa pamoja waliishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na
kusema kwamba ndiyo ilikuwa chanzo kikuu cha kuvuruga wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Wanasiasa hao waliweka bayana kwamba majeraha wanayoyajadili yasingekuwepo kama Nec ingefuata taratibu zote na kuacha kupokea maelekezo kutoka upande wowote wala chama chochote cha siasa.
Kikubwa walichosema katika mjadala huo wa siku moja ambao ulihusisha wawakilishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Bara (Nec) na ile ya Zanzibar (Zec), wanasiasa kutoka nchi jirani ya Uganda, viongozi wa Kituo cha Demokrasia Nchini TCD ni kwamba mapungufu ya Katiba ya nchi yalichangia kuzua matatizo hayo.
Katika kukabiliana na kutibu majeraha hayo wanasiasa wengi walishauri kwamba serikali iharakishe upatikanaji wa Katiba mpya kwa madai kuwa itasaidia kuondoa kasoro zote ikiwemo kuweka bayana muundo wa tume.
Akitoa mchango wake katika mjadala huo, mwakilishi kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Victor Kimesera anasema Nec inapaswa kulaumiwa kwa kasoro zote zilizojitokeza.
Kimesera anasema viongozi wa Nec waliamua kupindisha sheria na taratibu za uchaguzi kutokana na maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatua ambayo imeacha majeraha na kuifanya jamii kupoteza imani kwa serikali yao.
Anaongeza kuwa Wananchi wengi walikosa imani na Nec kutokana na madudu iliyoyafanya mwaka jana kwa lengo la kukifurahisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema.
Mbali na Nec lakini pia Kimesera anasema Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa naye alihusika kuvuruiga uchaguzi huo ambapo aliingilia majukumu ambayo yalikuwa yasiyomhusu ikiwemo kujigeuza kuwa msimamizi wa vyama vya siasa wakati jukumu lake ni kusimamia usajili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahimu Lipumba, akizungumza katika mkutano huo wa siku moja anasema mwaka jana Nec ilishindwa kusimamia Uchaguzi Mkuu na kuufanya uwe huru na haki.
Profesa Lipumba anasema chanzo cha matatizo hayo ni kukosekana kwa Katiba mpya ambayo ingeweza kuunda tume huru inayojitegemea badala ya sasa ambapo kila kitu kinafanywa na serikali iliyopo madarakani.
Ili kukabiliana na kudhibiti tatizo hilo lisitopkee tena anawashauri wanasiasa kudai kwa nguvu zote Katiba mpya ambayo anasema ndiyo itakuwa msingi wa kupatikana tume huru.
Anasema wakati umefika wa kuitazama Nec kwa mapana ili kuondoa migogoro na migongano isiyokuwa ya lazima kila unapofika Uchaguzi Mkuu.
Katika kuhakikisha hilo linawezekana na kukamilika anamuomba Rais Jakaya Kikwete kuweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa kusimamia uandikaji wa Katiba mpya pamoja na upatikanaji wa Tume huru ya Uchaguzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha United Democratic (UDP), John Nkolo, akitoa mchango wake katika mjadala huo anasema nafasi za viongozi wa Nec zitangazwe na kamati maalumu iteuliwe na Bunge ili kusimamia uchambuzi wa majina yao kabla ya kupeleka kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa mwisho.
Anasema hatua hiyo itasaidia Nec kuacha kufanya kazi kwa shinikizo la mtu ama chama chochote cha siasa ikiwemo CCM.
Anataka Nec ipewe sheria ya kudhibiti vyombo vya habari ambavyo wakati wa uchaguzi hukipendelea CCM huku vyama vingine vidogo vikiachwa pembeni.
Naye Mkuu wa Mambo ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa wa CCM, January Makamba, akizungumza katika mjadala huo anasema majeraha ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana yalitokana na uchanga wa kuwepo mfumo wa vyama vingi hapa nchini.
Makamba anasema njia pekee ya kuondoa majeraha ni kwa kila chama kujiona kwamba hakipo sahihi kwa asilimia 100 na kukubali kujikosoa na kukosolewa ili kipindi kijacho yasiweze kutokea tena.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, John Tendwa, anakiri kwamba katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka jana vyama vya upinzani vilikishika pabaya CCM tofauti na vipindi vingine vilivyopita.
Anasema kutokana na hatua hiyo baadhi ya sheria zilipindishwa na kuvurugwa ingawa ofisi yake ilihakikisha vyama vyote vinapata haki sawa ya kushiriki katika uchaguzi.
Tendwa anasema mwaka jana wananchi wengi hawakupiga kura kama ilivyokusudiwa na kwamba hilo ni fundisho kwa Tanzania na kutaka jitihada kubwa ichukuliwe ili kurekebisha hali hiyo.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni

No comments:

Post a Comment