Saturday, May 21, 2011

UKWELI JUU YA CCJ HADHARANI

*Yumo pia Mbunge Victor Mwambalaswa
*Watajwa kuwa ndiyo waanzilishi wa CCJ
*Mwingine alibana fedha za pango, samani
*Nape adaiwa kuwa ndiye mtunzi wa Katiba

Na Mwandishi Wetu, Njombe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendeleza mashambulizi dhidi ya viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na safari hii kimewataja vigogo wanne kinaodai walishiriki kuanzisha Chama Cha Jamii (CCJ).
Mmoja wa makada wa Chadema, Fred Mpendazoe, ndiye aliyevishwa dhima ya kuwataja vigogo hao. Alitaja majina yao katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Njombe, jana.
Waliotajwa kwamba walihusika kuanzisha CCJ ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM); na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye.
Alisema yeye alikuwa pamoja na viongozi hao wakati wa kuanzishwa kwa CCJ, na walikubaliana kuwa kwa pamoja waihame CCM.
Hata hivyo, kwa kile alichokiita kuwa ni unafiki wa viongozi hao, alitelekezwa na wenzake hao na kujikuta akijitangaza yeye peke yake kuwa ni mwanachama wa CCJ.
Wakati akihamia CCJ, Mpendazoe alikuwa Mbunge wa
Kishapu mkoani Shinyanga kupitia CCM. Kwa kuhamia CCJ, alipoteza ubunge.
“CCM wanafiki, ndani ya CCM ni unafiki, hawa watu walianzisha chama kingine, sasa wengine ni wabunge, wengine mawaziri na wengine viongozi ndani ya CCM, ni wanafiki.
“Tulikubaliana tuhame wote, lakini kwa sababu ni wanafiki, hawakuondoka kama mimi,” alisema na kushangiliwa.
Aliongeza, “Nape anajifanyaje mzalendo wakati alianzisha chama kingine?”
Alisema mmoja wa viongozi hao aligoma kujiunga CCJ, lakini akabaki na fungu nono la fedha zilizokuwa zimetolewa na wafadhili kwa ajili ya kuendeshea chama.
Alisema fedha hizo zilikuwa maalumu kwa ajili ya kulipia kodi ya pango la ofisi na ununuzi wa samani. Hakutaja kiasi cha fedha kilichotafunwa na kigogo huyo.
Alirejea kauli aliyoitoa hivi karibuni kwa kusema kwamba Nape ndiye aliyejihusisha na ukusanyaji katiba za vyama mbalimbali barani Afrika ili kupata katiba ya CCJ iliyo bora zaidi.
Nape anadaiwa kwamba baada ya kushindwa kwenye kura za maoni katika Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam, alikwenda Chadema kuomba apewe nafasi ya kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho cha upinzani.
Mwanasheria na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, wiki iliyopita alisema kwamba chama hicho baada ya kutafakari, kiliona Nape hana sifa za kumzidi John Mnyika, aliyekuwa amepitishwa kuwania ubunge na hatimaye kushinda.
Kwa upande wake, Nape alikanusha madai hayo na kusema kwamba Chadema ndiyo waliokuwa wa kwanza kumfuata ajiunge nao baada ya kushindwa kwake kwenye kura za maoni.
Tangu awali, kulikuwapo maelezo ya wazi mitaani kwamba Sitta na Mwakyembe ni miongoni mwa waanzilishi wa CCJ. Hata hivyo, viongozi hao mara kadhaa walinukuliwa wakipuuza madai hayo.
Wakati CCJ inaanzishwa, Sitta alikuwa Mbunge wa Urambo Mashariki na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dk. Mwakyembe alikuwa Mbunge wa Kyela; ilhali Mwambalaswa alikuwa Mbunge wa Lupa. Wote bado wanashikilia nafasi za ubunge kwenye majimbo yao.
Aidha, Sitta na Mwakyembe wakiwa bungeni walikuwa miongoni mwa kundi lililojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi wakitiwa nguvu na wabunge kama Mpendazoe.
MTANZANIA lilikuwa gazeti la awali kabisa kuandika kuwa CCJ kilikuwa chama kilichokuwa kimeasisiwa na vigogo kutoka ndani ya CCM. Kuandikwa kwa habari hizo kulielezwa na wachunguzi wa mambo kuwa ndiko kulikotibua mipango ya vigogo wengi kujitangaza hadharani.

About the Author

admin has written 1920 stories on this site.

Write a Comment

Gravatars are small images that can show your personality. You can get your gravatar for free today!









Get a new challenge
Get an audio challenge
Help


Copyright ©2011 Newhabari.

No comments:

Post a Comment