Festo Polea
MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika shule moja ya msingi ya jijini Dar es Salaam, inayotoa elimu yake kwa lugha ya Kiingereza, amejeruhiwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuchapwa bakora akiwa uchi.
Habari zilidai kuwa kitendo hicho dhidi ya mwanafunzi wa kike, kimefanywa na mhudumu wa usafi katika mabweni ya watoto.Inasemekana kuwa mtoto huyo alichapwa Juni 14 mwaka huu, baada ya kukataa kufua nguo yake ya ndani, aliyoikuta ikiwa imetapakaa kinyesi cha mtu ambaye hakufahamika.
Kubainika kwa ukatili dhidi ya mtoto huyo, kumekuja baada ya mama yake mzazi, Teddy Salimwe, kuamua kumtembelea Juni 20 mwaka huu kwa lengo la kumjulia hali.Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Teddy alisema alipokutana na mtoto wake, aliamua kumpakata lakini mtoto alikuwa analia kwa maumivu makali yaliyotokana na majeraha.
Alisema baadaye alimdadisi mtoto huyo, ili kujua kilichompata na kwamba katika maelezo yake, mtoto alidai kuwa alikuwa amechapwa bakora na mhudumu wa usafi.
Alisema baada ya maelezo hayo, alimwendea Mwalimu mkuu ili kupata maelezo ya kina kuhusu sababu za mtoto kutendewa ukatili huo.Kwa mujibu wa Teddy, kiongozi huyo wa shule, alimwelekeza kwenda kwa msaidizi wake ambaye hata hivyo, alishindwa kutoa maelezo na badala yake, alimtaka kuondoka na mtoto kama alihisi kuwa adhabu aliyopewa hakustahili.
Alisema kauli ya mwalimu huyo msaidizi, haikunifurahisha jambo lililomlazimisha kurudi kwa Mwalimu mkuu ili kupata ufafanuzi zaidi, lakini naye hakuonyesha ushirikiano.Teddy alisema kitendo hicho kilimsukuma kwenda polisi ambako alitoa taarifa na kupewa RB yenye namba STK/RB/8990/11.
Akisimulia chanzo cha kuchapwa bakora, mtoto huyo alisema ni kukataa kufua nguo yangu ya ndani niliyoikuta ikiwa na kinyesi kitandani kwangu, sikumjua aliyeitumia kujifutia kinyesi chake."
Alisema pamoja na jitihada zake za kujitetea, mhudumu wa usafi alimchapa kwa kutumia bakora maalumu kwa madai kuwa ni mjeuri.""Alinichapa kwa muda mrefu kwa kutumia fimbo ya 'Mr Bluu, nililia sana tena kwa sauti kubwa ambayo naamini wanafunzi wote walisikia nilivyokuwa nikichapwa huku nikiwa uchi,'' alidai mtoto huyo.
Alidai kuwa baada ya kumchapa, mhudumu huyo alimtaka aisitoe kwa mtu yeyote, taarifa kuhusu kipigo hicho, jambo lililomfanya aendelee kulia kwa maumivu yaliyomfanya ashindwe kutembea wala kufanya chochote.
Mwandishi wa habari hii alimtafuta Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Nashon Fanuel Rhobi na kumuuliza kuhusu tukio hilo.Katika majibu yake, kiongozi huyo wa shule alisema alikuwa hafahamu kama mtoto huyo alikuwa amejeruhiwa kwa kiasi hicho.
Ofisa Habari wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (WLAC), alisema chama hicho kimepokea taarifa kuhusu ukatili huo na kwamba inazifanyia kazi. |
No comments:
Post a Comment