Tuesday, June 7, 2011

Rais Saleh wa Yemen 'aliumia' sana


Saleh
Rais wa Yemen Ali Abdallah Saleh anayedaiwa kujeruhiwa vibaya
Rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, alijeruhiwa zaidi katika shambulio la makombora katika boma lake juma lililopita kuliko ilivyodhaniwa, maafisa wa Serikali wameambia vyombo vya Habari vya Marekani.
Maafisa wa Serikali waliambia shirika la Habari la AP kuwa Bwana Saleh alichomeka asilimia 40 ya mwili wake na anavuja damu katika fuvu lake kutokana na shambulio hilo la Ijumaa.
Rais anaendelea kupata matibabu nchini Saudi Arabia baada ya kushambuliwa katika Ikulu yake katika Mji Mkuu wa Yemen, Sanaa.
Afisa wa cheo cha juu Serikalini aliambia BBC kuwa hawatasema lolote kuhusiana na afya ya Rais Saleh.
"Sisi si madaktari. Na kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Bi Hillary Clinton alivyosema jana, sisi tuko hapa na Sanaa na tunafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa tunaleta mabadiliko kwa utaratibu, amani na
bila ghasia, kama inavyosema Katiba ya Yemen," afisa huyo alisema.

Uwezo wa kutawala


Kaimu kiongozi, Makamu wa Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi, alisema Bwana Saleh anatarajia kurejea baada ya siku chache.
Lakini wachunguzi wanasema kuwa kiwango cha majeraha ndicho kitakachoamua ni lini - na ikiwezekana - ikiwa atarudi katika taifa hili lenye umuhimu mkubwa ambalo amelitawala kwa zaidi ya miaka 33. Hali hiyo pia itaamua ni nani atakayechukua mamlaka iwapo yeye hatakuwa na uwezo wa kutawala.

Jaribio la kutaka Kuua

Haikujulikana kiwango cha alivyochomeka na kiwango cha majeraha alichokuwa nacho lakini Jumamosi wandani kadhaa wa Rais Saleh walisema kuwa alichomeka kwenye kifua na uso na kwamba mabaki ya kombora yalipenyeza chini ya moyo wake.
Rais alifanyiwa upasuaji Jumatatu ili kuondoa vipande vya mbao katika kifua chake na pia kumtibu majeraha ya moto kwenye uso na kifua, kama shirika la AP linavyoripoti.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 69 hajaonekana tangu Ijumaa wakati makombora yalipotumika kushambulia Ikulu ya Rais na kuwaua watu saba na kuwajeruhi maafisa kadhaa wa vyeo vya juu Serikalini katika tukio ambalo maafisa hao wa Serikali wanasema ni jaribio la kutaka kuwaua.

No comments:

Post a Comment