Tumepokea kwa masikitiko makubwa propaganda za CCM kuwa chama chetu kunatumia fedha kuwalipa Wananchi kufanikisha maandamano tunayoyaratibu. Propaganda hizi zimepewa uzito sana hata na baadhi ya vyombo vya habari vichache ambavyo ama ni vibaraka tu wa CCM au vina maslahi ya moja kwa moja katika hali ya ufisadi ambavyo inaendekezwa na CCM na kupingwa na CHADEMA.
Baadhi ya Mawaziri wa serikali ya Rais Kikwete hususan Mzee Steven Wasira, Sofia Simba na Bernad Membe nao wameingia katika upofu huo. Huu ni upofu kwa kuwa Wasira aliyaona maandamano ya Mwanza. Ukiwa na akili ya kawaida utajiridhisha kuwa huwezi kuwa na njia yeyote ya kuweza kulipa hadhira ile.
Kwa tamko hili tunapenda ifahamike kwa kila mmoja kuwa CHADEMA haimlipi yeyote kuandamana, haijafanya hivyo na haitafanya hivyo. CHADEMA inaamini kuwa maandamano haya ni
harakati za wananchi kudai haki zao. Kwetu sisi (CHADEMA) haiingii akilini kuwa yupo mwananchi mmoja anayeweza kufikiria kulipwa ili adai haki zake.CHADEMA inasisitiza kuwa tutaendelea kuratibu maandamano haya mpaka yakamilike Nchi nzima. Aidha ifahamike pia kuwa tunachukua maoni yote yanayotolewa katika maandamano na mikutano tunayofanya kwa kuwa ni maoni ya wenye Nchi yao na ni lazima yasikilizwe na serikali yoyote inayotaka uhalali kwa watu wake.
Ni vema ikaeleweka kwa watu wote kuwa wote wanaoeneza uvumi eti CHADEMA inapewa fedha na mataifa ya Nje kuendesha maandamano kwa lengo la kuvunja amani kuwa wana fanya hivyo kwa malengo yao binafsi yenye nia ya kudhoofisha jitihada zinazoratibiwa na CHADEMA. Kwa wale ambao maandamano hayajafika kuwa tunatoa mwito wajitokeze na wachukue taadhari zote na wale wote wenye lengo la kuvunja amani ili kupaka matope maandamano hayo. Kujitokeza kwa wingi na kwa amani kutapeleka ujumbe kwa watawala kuwa ghiliba zao zimeshindwa; njia pekee kwa serekali ni kutoa suluhisho kwa hoja zinazotolewa. CHADEMA haitaacha kuongoza wananchi kudai haki zao kwanza kwa kuwa sisi wenyewe, Viongozi wa CHADEMA, ni sehemu yao na matatizo yanayosababishwa na uongozi uliopo yanatuhusu pia na pili ni wajibu wetu wote kuzuia matumizi mabaya ya Raslimali za nchi yetu.
Wananchi wameandamana maelfu kwa maelfu katika mikoa minne na wilaya zake; wao ni mashuhuda kuwa hayupo hata mmoja aliyelipwa chochote ili aandamane.
Tunashangazwa na majeshi yetu, masuala tunayotuhumiwa nayo ni mazito eti tunataka kupindua serikali halali, tunapewa pesa toka nje na tunawalipa watu kuandamana kuvuruga amani. Majeshi yote yanapaswa kuchukua hatua. Jeshi la ulinzi lina wajibu wa kulinda nchi yetu dhidi ya mataifa mengine. Sofia Simba na Membe wamesema tunapewa pesa na mataifa ya nje. Jeshi letu litake msaada wao ili ukweli ubainike. Idara ya usalama wa Taifa na polisi mbona kimya? Tuelewe nini? Kuwa Mawaziri ni waongo, wanaropoka tu, kauli ambazo zinayumbisha wananchi na kuiletea Nchi yetu maswali mbele ya jamii ya kimataifa halafu waendelee kuwa Mawaziri? Au ni kweli CHADEMA inatumika kuvuruga amani ya Nchi?
Sisi katika CHADEMA tunakana uvumi huo. Tuko tayari kutoa ushirikiano kwa majeshi yetu kuona mahesabu yetu na “mienendo ya “Bank accounts” zetu. Tunataka majeshi yetu yachukue hatua haraka.
Sisi katika CHADEMA tunakana uvumi huo. Tuko tayari kutoa ushirikiano kwa majeshi yetu kuona mahesabu yetu na “mienendo ya “Bank accounts” zetu. Tunataka majeshi yetu yachukue hatua haraka.
Mwisho: tunapenda tueleweke kuwa sisi ni wazalendo, tunaipenda Nchi yetu, tunapenda iongozwe vizuri na watu wenye hadhi na mapenzi kwa nchi yenyewe na watu wake.
Pamoja na salaamu za CHADEMA.
Anthony Calist Komu
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala
Kny. Katibu Mkuu.
Kny. Katibu Mkuu.
No comments:
Post a Comment