venance.chadema@yahoo.com
Monday, 18 July 2011 21:34 |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeunda tume itakayoongozwa na Profesa Abdallah Safari kumhoji Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu zinazomkabili.
Hii ni mara ya pili kwa Shibuda kuhojiwa na jopo maalumu la Chadema kwani tayari aliwahi kuhojiwa baada ya kupingana na msimamo wa chama hicho wa kumsusia Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizundua Bunge Desemba mwaka jana kwa kuhudhuria dhifa katika Ikulu ya Chamwino huku akiweka bayana kupingana na msimamo huo.
Mapema mwezi huu alitoa tena kauli ambazo Chadema imeziita ni zenye kukiuka maadili hali iliyomfanya Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje, John Mnyika kuwasilisha malalamiko rasmi ndani ya Kamati Kuu (CC).
Akizungumza Dares Salaam jana baada ya kikao cha CC, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hatua ya kuunda tume kwa ajili kufanya kazi ya kupitia tuhuma hizo imetokana na madai ya mlalamikaji kuwa na mantiki.
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Edson Mbogoro, Said Mzee, Lazaro Masey na Ester Daffi ambaye si mjumbe wa kamati, bali atafanya kazi kama mratibu wa kamati hiyo akitokea Ofisi ya Katibu Mkuu.
Dk Slaa alisema: “Kikao cha kamati kilichokaa jana (Juzi) hakikujadili suala la Shibuda na mambo yaliyopo bungeni, bali kilipokea taarifa ya malalamiko kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu juu ya kitendo cha Shibuda kukiuka maadili. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ili hatua ziweze kuchukuliwa kwanza ni lazima malalamiko yawasilishwe Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama naye kuyawasilisha kwenye Mkutano wa Kamati Kuu.”
Dk Slaa alisema malalamiko yalipokewa na kamati kuu na kisha kujadiliwa na kuona kuna hoja ya kufanyiwa kazi. Yaliwasilishwa ofisini kwake Julai 14, mwaka huu na Mnyika.
Alisema msingi wa malalamiko hayo hautokani na kile kilichotoea bungeni, bali kitendo cha mbunge huyo kukaririwa na vyombo vya habari akitoa tuhuma dhidi ya viongozi wa chama hicho hadharani kinyume na utaratibu.
Alisema Chadema kinafuata kanuni taratibu na sheria ambazo zimeundwa kwa muda mrefu sasa na kusisitiza sheria hizo hazikutungwa kwa ajili ya mtu Fulani, bali kuwezesha wanachama wote wakiwamo viongozi kufuata taratibu.
“Sheria za Chadema ziko wazi tume iliyoundwa na Kamati Kuu itafanya kazi zake na kuwasilisha ripoti yake mara itakapomaliza kazi hiyo na kutoa mapendekezo ya kuchukua. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, kamati hiyo haina mamlaka ya kutoa uamuzi hivyo itawasilisha mapendekezo yake kwenye Kamati Kuu kwa hatua zaidi,”alisema Slaa.
Kuhusu hatua ya Shibuda kutofautiana na kauli ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni kuhusiana na suala la posho, alisema hilo lina taratibu zake na kusema kwamba kamati ya kambi ya upinzani bungeni inalishughulikia.
Madiwani Arusha
Akizungumzia suala la madiwani wa Arusha, Dk Slaa alisema Kamati Kuu imetengua maridhiano hayo na kuwaagiza madiwani wake kujiuzulu nyazifa zote walizozipata kinyume na utaratibu.
Alisema Kamati Kuu imebariki hatua hizo kwa kuzingatia kuwa lengo la Chadema kugomea uchaguzi wa meya si kutafuta nafasi ya naibu meya, bali kupinga kitendo cha kutofuatwa kwa sheria za mchakato wa uchaguzi huo.
“Chadema hatuna njaa ya unaibu meya wala uenyekiti wa kamati, sababu za kupinga uchaguzi huo ni kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi, Kamati Kuu imekataa maridhiano hayo na leo (jana), ninawaandikia barua madiwani nikitaka wajiuzulu nafasi hizo zilizopatikana kinyume na utaratibu,” alisema Slaa.
Slaa alisema Katiba ya Chadema iko wazi na kama mtu atapingana na uamuzi huo hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yake. “Milango iko wazi, kama mtu anaona hawezi kufuata taratibu na mfumo tulionao anaweza kuhamia chama kingine” alisema Slaa. |
No comments:
Post a Comment