Thursday, July 14, 2011

Ni uamuzi mgumu, utapeli au ajali ya kisiasa?






Printer-friendly versionSend to friend Waziri Mkuu Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amelidanganya tena Bunge. Amedai serikali ya awamu ya nne imefanya maamuzi mengi magumu kuliko serikali nyingine yoyote iliyotangulia. Hii ni kejeri ya aina yake na ninaamini rais mstaafu Benjamin Mkapa alipomsikia Pinda akitoa kauli hiyo alishikwa na bumbuwazi.
Moja ya maamuzi aliyoyataja wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge, ni ule wa kuvunja baraza la mawaziri na kuliunda upya. Huku akiwatolea macho wabunge wenzake, Pinda alisema
uamuzi huo ulikuwa mgumu na kuwa “inahitaji moyo” kufanya hivyo.
Mengi yasememwa kuhusu hoja hii. Nami napenda nishiriki pia kwa kuweka bayana kwamba Rais Jakaya Kikwete hakuvunja baraza la mawaziri Februari 2008. Bali, Edward Lowassa ndiye aliyelivunja baada ya kujiuzuru akidai anawajibika kwa ajili ya serikali yake na chama chake.
Hata kama hatima ya yote ni juu ya rais kukubali au kukataa uamuzi huo, bado si rais aliyevunja baraza hilo, bali ni Lowassa aliyejiuzuru na kusababisha baraza zima kuvunjwa.
Kwa kuwa suala hili linajadilika, ni nafuu pia kusema serikali ile ilivunjwa kutoka na “utapeli” wa kisiasa wa Rais Kikwete kwa swahiba wake Lowassa, kuliko kusema serikali hii ilifanya uamuzi mgumu wa kuvunja baraza la mawaziri.
Kuna ukweli umesemwa muda mrefu, na kwa kuwa serikali wala rais wake hawajaukanusha, inabidi ubaki katika kumbukumbu halisi za nini hasa kilitokea Februari 2008 mjini Dodoma.
Bunge kupitia Kamati Teule ilisoma ripoti yake kupitia mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe. Hali ilikuwa tete Dodoma na hata Chamwino ambako Rais Kikwete alikuwa amejichimbia.
Baada ya kusomwa kwa ripoti, taarifa zinasema Lowassa alikwenda Chamwino kuonana na bosi wake ili kupanga mkakati wa kuzima maasi ya wabunge wa CCM waliokuwa wamesisimka ili kummaliza Lowassa, rais Kikwete na serikali yao.
Katika mazungumzo yao usiku ule, Rais Kikwete na swahiba wake huyo wa zamani – Edward Lowassa – walipima upepo na kuona pendekezo la Lowassa kuwa rais aende upesi kukutana na wabunge wa CCM ili kuwaonya wasiiangushe serikali yao, lilionekana halifai kwa hofu ya mihimili hiyo miwili kuingiliana.
Ndipo mpango ukasukwa kuwa Lowassa aandike barua ya kujiuzuru, lakini rais aicheleweshe kuijibu na Bunge lihairishwe ili kumpa nafasi rais kuonana na wabunge wa CCM ili kuzima maasi ya wabunge kabla ya mkutano mwingine wa Buge wa Aprili haujafanyika Dodoma.
Mpango ukakubaliwa na bila ajizi Edward Lowassa aliamini na kuandika barua ya “kuigiza” kujiuzuru na kisha akaondoka kurudi Dodoma mjini usiku ule. Yaliyotokea Chamwino baada ya Lowassa kuondoka inabakia kuwa siri ya Kikwete mwenyewe na aliokutana nao.
Usiku wa manane wa siku hiyo, Rais Kikwete aliamua kuwa barua ile ijibiwe na kukubaliwa. Ni kinyume na makubaliano yake ya awali na Lowassa. Huu diyo waziri mkuu Pinda anaita uamuzi mgumu.
Kwamba rais “kumtapeli waziri mkuu wake, na sasa waziri mkuu mwingine anaita hatua hiyo ni uamuzi mgumu? Pinda anayajua vema haya kwa kuwa wakati huo, alikuwa waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (TAMISEMI) chini ya Lowassa.
Ni mapema mno kuchunguza ni kwa kiasi gani Pinda alihusika katika sakata hili, na ni mapema mno kujiuliza Lowassa alihusika kiasi gani katika kumshauri rais Kikwete amteue Pinda kuwa waziri mkuu. Yote mawili yanachunguzika na siku zijazo tutawajuza.
Lakini kilichowazi, siku tatu baadaye, Rais Kikwete huyo huyo aliwaambia wazee wa jijini Dar es Salaam kuwa ile ilikuwa ajali ya kisiasa. Hakufafanua ana maana gani, lakini haiwezekani uamuzi mgumu ukawa ni ajali ya kisiasa.
Wapo wanaosema, Pinda anacheza na fimbo inayoweza kumpiga hata yeye. Haitarajiwi rais wa nchi awe “tapeli” hata kama utapeli wenyewe ni wa kisiasa dhidi ya kiongozi mwenzake katika chama kile kile na kisha hiyo aiite ajali ya kisiasa.
Mpaka hapa, bado si sahihi kwa Pinda kudai serikali ilifanya uamuzi mgumu wa kuvunja baraza la mawaziri wakati anayedaiwa kuvunja alisema hadharani kuwa ile ilikuwa ni ajali ya kisiasa.
Inaweza kuwa karibu na sahihi tukisema bunge lilivunja serikali kwa sababu kuu mbili.
Kwanza, ni Bunge lililounda kamati maalum kuchunguza kashfa ya Richmond. Hata kama kulikuwa na mashauriano ya nyuma ya pazia kati ya spika na Rais Kikwete, hayakuwa rasmi bali kinachojulikana ni kuwa Bunge liliunda kamati ya kuchunguza kashfa ya mkataba tata wa Richmond.
Kamati ile ilipomaliza uchunguzi wake ilisoma mapendekezo yake na kusema, Lowassa apime uzito wa tuhuma zinazomwelekea na aamue mwenyewe. Hata kama kamati ingesema kwa mkazo kuwa waziri mkuu ajiuzuru na akafanya hivyo, bado huu usingekuwa uamuzi wa serikali bali ni uamuzi wa bunge. Tungesema kwa uhakika kuwa bunge letu limefanya uamuzi mgumu, siyo serikali yetu.
Lakini mpaka hapa pia bunge halikumlazimisha Lowassa ajiuzuru, bali lilimshauri apime uzito wa tuhuma zile na afanye uamuzi wenye busara. Aliyelazimika kufanya uamuzi mgumu ni Lowassa siyo serikali wala Bunge.
Tunaweza kusema kwa ustaarabu na uvumilivu kuwa bunge lilisababisha kuvunjika kwa baraza la mawaziri pale lilipomshauri waziri mkuu apime na kuamua uzito wa tuhuma.
Na kwa uhakika tunaweza kusema, Edward Lowassa baada ya kupima ushauri wa Bunge alifanya uamuzi mgumu wa kujiuzuru na kusababisha baraza zima livunjike.
Hatuwezi kusema rais alivunja baraza. Tunachojua Rais “alikubali” kujiuzuru kwa Lowassa na mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha na ndipo baadaye kidogo akashtuliwa na mnikulu mmoja kwamba kujiuzuru kwa waziri mkuu kunavunja pia baraza zima.
Dokezo hili pia lilitolewa kwenye ukumbi wa bunge na mbunge Zitto Kabwe, asubuhi ya kujizuru kwa Lowassa. Rais Kikwete anajua kuhusu barua ya maigizo ya kujiuzuru Lowassa. Kwamba hakuwa anajua kuwa kujiuzuru kwake kunavunja baraza zima.
Mmoja wa wasaidizi wake aliyejiunga baadaye na serikali yake ameniambia kuwa, kama angejua asingekubali kwa sababu hatua hiyo imevunja hadhi ya serikali yake na yeye binafsi.
Pili, ni sahihi zaidi kusema Bunge lilivunja baraza la mawaziri kwa sababu iwe Edward Lowassa, awe Rais Kikwete wote mpaka leo wana hasira na aliyekuwa spika wa wakati huo Samwel Sitta.
Spika huyu ametuhumiwa na hatimaye kuadhibiwa na chama chake chini ya uongozi wa Kikwete kwa kuondolewa katika nafasi yake aliyoipenda na kuimudu. Viongozi wote wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanadai mpaka leo kuwa Sitta anahusika na anguko la serikali ile na kushuka kwa umaarufu wa Kikwete, Lowassa na CCM kwa ujumla wake.
Ni suala la muda tu, siku moja tutashuhudia kusulubishwa kwa Sitta ili kulipa kisasi cha mateso anayodaiwa kuisababishia chama chake na viongozi wake. Hata Sitta analijua hili vema na atafanya makosa makubwa sana akikubali kudanganywa na nafasi ya uwaziri aliyopewa ili asahau kitanzi kinachomsubiri.
Kama Pinda anasema ukweli juu ya serikali kufanya maamuzi magumu ya kuvunja baraza la mawaziri, kwa nini Sitta achukiwe mpaka leo? Kwa nini aliondolewa katika nafasi yake baada ya kuhojiwa mara mbili ndani ya vikao vikuu vya CCM?
Kimsingi, haiwezekani serikali ikafanya uamuzi mgumu wa kuvunja baraza na hapo hapo Spika Sitta akachukiwa kwa kusababisha serikali kuvunjika. Haiwezekani kuwapo kwa makundi ya kulipizana visasi, wala njama za kutaka kufukuzana ndani ya chama. Haiwezekani!
venance.chadema@yahoo.com

No comments:

Post a Comment