Wednesday, August 17, 2011

Kago ruksa leo

venance.chadema@yahoo.com

 
Tuesday, 16 August 2011 20:16


SHIRIKISHO la Soka Tanzania ( TFF) limesema kuwa linasubiri majibu kutoka kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuhusu klabu ya Simba kumtumia mchezaji wao mpya, Gervais Kago kama ataweza kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Kago aliyesajiliwa akitokea klabu ya Olympic Real de Bangui ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), amekuwa na utata wa kuichezea timu yake hiyo mpya baada ya kuchelewa kufika Uhamisho wake wa kimataifa (ITC) kupitia mfumo wa mtandao wa  Transfer Matching System (TMS).

Akifafanua suala hilo Mwenyekiti wa Kamati wa Sheria Maadili na Hadhi za wachezaji, Alex Mgongolwa alisema mchezaji huyo ameruhusiwa kucheza mechi ya Ngao ya Jamii kwa kuwa lengo lake ni kusaidia jamii na Pili ni kuzindua msimu mpya wa Ligi na tatu, Simba imeonesha nia ya kumhamisha kutoka CAR.

''FIFA ndio watakuwa na kauli ya mwisho ya kumruhusu mchezaji huyo kucheza au la baada ya kupitia mawasiliano ya Simba na timu ya  Olympic Real de Bangui kama yalikuwa kwa muda, lakini kwa upande wao hawataweza kumruhusu mpaka dirisha dogo la usajili kwa mujibu wa kanuni," alisema Mgongolwa.

Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 2(2) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirkisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), mchezaji wa kulipwa ni yule ambaye ana mkataba wa maandishi na klabu na analipwa kutokana na shughuli ya kucheza mpira.

Hata hivyo; Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa baada ya kuligundua hilo waliitaarifu klabu ya Simba ambayo nayo ilileta vithibitisho vya barua jana kuthibitisha kuwa walikuwa na mawasiliano na klabu ya mchezaji huyo kwa ajili ya kutoa ( ITC) mpaka sasa bado wako kimya.

Pia, Angetile alisema Simba iliiomba TFF, iwaruhusu wamtumie mchezaji huyo katika ligi mpaka ( ITC) itakapowasili kitu ambacho kanuni za FIFA haziruhusu.

Katika Hatua nyingine Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwa upande wao Simba wamefurahishwa na kitendo cha TFF kumruhusu mchezaji huyo kucheza mechi ya leo.

Hata hivyo alisema kutokana na kuchelewa kwa ITC klabu imeamua kumtuma Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage kwenda Afrika ya kati katika timu ya Kago kufuatilia kwa nini ITC hiyo imechelewa kufika mpaka leo pamoja na kuwa na mawasiliano.

Kamwaga pia alisema kuwa Athuman  Idd Chuji sio mchezaji wao kama TFF wanavyosema hivyo ni vyema  wamuachie akaangalie maisha yake kwani wao waliingia mkataba wa maangalizi ya miezi sita, lakini walishindwa na kumuachia.

No comments:

Post a Comment