Wednesday, May 25, 2011

JK achangia harambee ya Chadema 10m/

23rd May 2011
Chapa
Maoni
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ameahidi kutoa Sh. Milioni 10 kwa kuchangia Mfuko wa Maendeleo ya Elimu ya Jimbo la Nyamagana linaloongozwa na Mbunge Ezekia Wenje wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chandema).
Kikwete alitoa ahadi hiyo juzi usiku, katika hafla ya uzinduzi wa mfuko huo iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest jijini hapa.
Katika harambee ya kuchangia mfuko huo baada ya kuzinduliwa iliyoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, iliwezesha jimbo hilo kupata kiasi cha Sh. Milioni 50 licha ya kuhudhuriwa na watu wachache. Katika harambee hiyo, Zitto alipiga mnada sare yake iliyonunuliwa kwa Sh. milioni 1.7.
Baadhi ya vigogo wa vyama vya siasa waliopo ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza, waliwasilisha michango yao kwa Zitto kwa sharti la kutotajwa majina yao huku Kikwete akitoa ahadi hiyo kupitia kwa Wenje.
Kikwete alitoa mchango wake huo baada ya kumpigia simu Zitto akiwa anaongoza harambee hiyo iliyohudhuriwa na watu mbalimbali, kisha kumweleza jinsi alivyoguswa na mkakati huo wa maendeleo.
Rais aliahidi kuzituma fedha hizo kwa utaratibu utakaowekwa na
ofisi ya Wenje.
Wengine waliochagia harambee hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa Sh. Milioni 5, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe Sh. Milioni 2, Zitto Sh.Milioni 1 na Wenje Milioni 3.
Wabunge wengine wa Chadema waliotuma michango yao kwa kupitia kwa mgeni rasmi, Zitto ni pamoja na Gracy Kiwelu Sh. 300,000, Muhonga Said Sh. 200,000, Rayah Ibrahim Sh. 200,000 na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Charles Chinchibela (Chadema) Sh. 200,000.
Baadhi ya wafanyabiashara wa jijini Mwanza waliofanikisha harambee hiyo ni mfanyabiashara maarufu Joseph Madirisha aliyetoa Sh. Milioni 1 na wengine waliochangia kupitia Faceboock ya Zitto Euro 1,000 na 600,000.
Zitto aliwataka wanasiasa kuacha tabia ya kususia shughuli za maendeleo kwani wakati huu si wa siasa bali ni kupigania maendeleo ya wananchi wote kwa ujumla.
" Nasikitika sana kuona baadhi ya wanasiasa wanaogopa kujitokeza wala kuchangia maendeleo. Tunatakiwa tuweke siasa pembeni kama ambavyo mheshimiwa Rais Kikwete alivyoweka pembeni itikadi na kuchangia milioni 10.
Jimbo la Nyamagana lina shule za sekondari 28 zinazohitaji madawati 2,219.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment