23rd May 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Yahitimisha wameshindwa majukumu yao
Yapania kukwamisha bajeti ya Nishati
Yapania kukwamisha bajeti ya Nishati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imesema Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), William Mhando, ni mzigo kwa taifa kwa kuwa wamelidanganya Bunge, Rais Kikwete na wananchi kwa kutoa ahadi hewa kwamba mgawo wa umeme utamalizika kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Vile vile, Kamati hiyo imedhamiria kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 ikiwa serikali itashindwa kutoa majibu ya uhakika kuhusu kumaliza tatizo la mgawo wa umeme nchini.
Kadhalika, Kamati hiyo imetaka majibu juu ya mapendekezo 30 iliyotoa mapema mwaka huu kwa serikali na Tanesco ili kumaliza tatizo la umeme ikiwemo kukodi mitambo ya dharura itakayokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 260.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa viongozi hao wamekuwa wakikimbilia uchochoroni kujificha badala ya kutoa majibu kuhusu ahadi zao.
“Kufuatia kauli hizo za Ngeleja na Mhando, Rais naye alilitangazia taifa hivyo hivyo kwamba ufumbuzi wa mgawo wa umeme utapatikana mwezi Juni mwaka huu jambo ambalo limeshindikana,” alisema.
Makamba alisema serikali imezoea kutoa ahadi nzito kwa
wananchi, lakini mwisho wa siku inakuja na majibu mepesi kwa lengo la kujitetea na kuongeza kuwa safari hii kamati yake haitavumilia kusikia kauli za namna hiyo kutoka serikalini.
wananchi, lakini mwisho wa siku inakuja na majibu mepesi kwa lengo la kujitetea na kuongeza kuwa safari hii kamati yake haitavumilia kusikia kauli za namna hiyo kutoka serikalini.
“Kumekuwa na utamadini kwa serikali kutoa ahadi kubwa na nzito bungeni lakini mwisho wa siku inakuja na majibu mepesi ya kujitetea, lakini kamati yangu haitataka kusikia utetezi wa namna hiyo,” alisema. Alisema Ngeleja aliliahidi Bunge Februari mwaka huu kwamba ifikapo Juni Tanesco itakuwa imekodi mitambo ambayo ingekuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 260.
Makamba alisema ahadi hiyo ya Ngeleja iko katika kumbukumbu za Bunge (hansard), lakini kwa bahati mbaya imebakia wiki moja kufikia mwezi Juni lakini hakuna juhudi zozote za makusudi kukamilisha ahadi hiyo.
Alifafanua kuwa zabuni iliyotangazwa na Tanesco kwa ajili ya kupata makampuni ya kuagiza mitambo ya kuzalisha umeme ili kumaliza tatizo imegonga mwamba, lakini Ngeleja na Mhando hawajasema lolote.
Zabuni hiyo ilikuwa inagharimu Sh. bilioni 500 na makampuni 17 kati ya 22 yalijitokeza kuomba, manne tu ndiyo yalirudisha fomu za maombi, hata hivyo baada ya mchakato kukamilika yalinyimwa kazi.
Alisema makampuni hayo yote yalitaka yaiuzie Tanesco umeme utakaozalishwa kwa Sh.1,005 hadi 1,006 kwa uniti moja wakati shirika hilo linawauzia wananchi uniti moja kwa Sh. 125 hatua ambayo ilisababisha pande zote mbili zishindwe kuafikiana, lakini Makamba alisema mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyewahi kusimama na kutoa taarifa kwa umma.
Aidha, alitaka Tanesco kutoa majibu ni kwa nini mitambo miwili iliyoipa kampuni ya Songas ambayo inatumia mafuta na gesi haitumiki.
Alisema ana ushahidi kuwa mitambo hiyo ipo na kwamba kila mmoja unazalisha megawati 20, Tanesco ilitoa Dola milioni 1.5 kwa ajili ya kuikarabati na kuikabidhi kwa Songas, lakini cha ajabu mpaka sasa imekaa bila kutumika huku nchi inakabiliwa na giza.
Makamba pia alilishambulia Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC), kwa kuidanganya kamati yake kwamba visima vya Songas havina hitilafu yoyote, lakini baada ya miezi michache kupita imeonekana kuwa na matatizo ambapo hivi sasa vinafanyiwa ukarabati.
Aliahidi kuwa TPDC itaitwa mbele ya kamati ili kujibu kwa nini ilitoa kauli za uongo huku ikijua visima vya Songas vilikuwa na matatizo makubwa yaliyosababisha hivi sasa vifungwe.
Kuhusu kampuni ya Songas kuiuzia Tanesco umeme kwa kutumia Dola za Marekani, Makamba alisema jambo hilo halikubaliki.
Mwenyekiti huyo alisema ili kukabiliana na mgawo wa umeme kamati yake itaishauri serikali kuruhusu makampuni binafsi kuingia katika biashara ya kusambaza nishati hiyo ili kushindana na Tanesco ambayo alisema imeshindwa kazi yake kwa kiasi kikubwa.
Alisema Songas wanaibia serikali fedha nyingi kutokana na mikataba mibovu iliyoingia na kwamba yeye haogopi kusema chochote na kutaka siasa iondolewe katika suala la kupata suluhisho la mgawo wa umeme.
Leo kamati hiyo inaanza vikao vyake, katika wiki ya kwanza itataka kupata majibu kutoka serikalini na Tanesco juu ya hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na mgawo wa umeme nchini.
Alipotafutwa kuzungumzia kauli ya Makamba, Ngeleja simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa wakati Mhando simu yake ilikuwa haipatikani.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni