Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema Kizitto Noya, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema jana alijikuta kwenye mgogoro na wabunge baada ya kueleza bungeni kuwa baadhi yao wanazungumza bila kufikiri ili waonekane kwenye luninga.
Tukio hilo lilitokea jana wakati Bunge limekaa kama kamati kupitisha Muswada wa Fedha wa mwaka 2011 ulioletwa bungeni kwa mara ya pili na Naibu wa Waziri wa Fedha na Uchumi, Pereira Silima .
Chanzo cha mgogoro huo ni mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuleta mapendekezo katika kifungo cha tano cha Muswada huo kutaka Kamishna na watendaji wa Serikali kuondolewa madaraka ya kusamehe kodi.
Lissu alilieleza Bunge kuwa tabia hiyo ndiyo mwanzo wa rushwa na ufisadi nchini kwani baadhi ya watendaji hao wamekuwa wakitumia vibaya mamlaka hizo. Lissu alitaka anayekosea katika suala la kodi akutane na adhabu.
Baada ya mapendekezo hayo, Mwenyekiti Anne Makinda alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutolea ufafanuzi suala hilo na Jaji Werema alisimama na kusema:
"Sina nia ya kutukana mtu, lakini niseme tu hilo liko wazi, kwamba mtu anayeweza kuchelewa kulipa kodi, lakini ana sababu na sasa tunasema ikitokea ana sababu za maana, asamehewe, hatuwezi kusema kwa sababu amekosea basi aadhibiwe, tunaishi na jamii ambayo watu wana matatizo,"
Aliendelea,"Nisema tu kwamba watu tusizungumze tu ili tuonekane kwenye luninga, nadhani ni vema tukafikiri kwa mapana na vizuri zaidi."
Kauli hiyo ilimwibua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye alisimama na kuomba mwongozo wa spika kisha akasema,"Mheshimiwa Spika humo ndani sisi ni viongozi na tuko kwenye legislation process. Sasa kuna kauli za kuudhi zinazotolewa na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambazo hazivumiliki"
Aliendelea,"Mimi namheshimu sana Jaji Werema, lakini siamini kwamba kauli hizo ni zake, labda awe ameumwa siku hizi mbili tatu. Kusema wabunge hatufikiri sawa sawa anatutukana wabunge, namwomba awaheshimu wabunge na afutee kauli yake kwamba wabunge wanazungumza ili waoanekane kwenye TV."
Akitolea mwongozo suala hilo, Makinda alisema "Nashukuru kwamba sasa kadiri siku zinazoendelea wabunge tunajua kuwa kuna maneno ya kauudhi maana wengine maneno hayo mnayatoa hata kwenye vyombo vya habari. Ni kweli kauli hiyo ya (Werema) inaudhi na tunamwomba aifute."
Baada ya agizo hilo, Jaji Werema alisimama na kusema kuwa "Mimi sijaumwa, ni mzima kabisa."
Baadaye Zitto alisimama na kusema "Nakubali Jaji Werema hajaumwa na nafuta kauli yangu."
"Sasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali simama na ufute kauli yako," aliagiza Makinda
"Naitoa kauli yangu," alisema Jaji Werema.
Hoja ya posho yatikisa Bunge
Hali iliendelea kuchafuka bungeni baada ya hoja ya posho kurejeshwa tena kinyemela na kuzua mjadala mkali kati ya wabunge wa CCM ambao waliendelea kutetea posho hizo na wabunge wa upinzani ambao wanaipinga.
Kauli ya Lissu kwamba mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono anaokoteza maneno kwa kutetea posho za wabunge akisema zipo hata kwa madiwani, ilizua balaa nyingine baada ya wabunge wengi wa CCM kusikika wakipiga kelele,"afute kauli hiyo afute!
Hata hivyo, Mwenyekiti Makinda alipuuza kauli hizo na kuendelea kuongoza mkutano huo huku wabunge wakiendelea kupigana vijembe chinichini.
Lissu alipinga pendekezo la Serikali kufuta kodi ya posho akisema sio sahihi kwani baadhi ya watumishi wa umma wakiwamo wabunge wanapewa posho kubwa inayostahli hata kukatwa posho.
Baadaye Waziri katika Ofisi ya Rais, (Sera na Utaratibu), William Lukuvi alisimama na kueleza kuwa hoja ya upinzani ni ya msingi, lakini inahitaji muda kufanya marekebisho hayo.
"Hoja hii ni sahihi, wabunge ni kweli tuna mishahara mikubwa kuliko watumishi wetu mimi napata responsibility allowance ya 200,000 na kiongozi wa upinzani anapata Sh2 milioni, ni vizuri, lakini tunahitaji kutumia kanuni kujadili hilo,"alisema
Lissu alieleza kuwa hoja yake sio kufuta posho bali kuondoa kodi ya posho wakati sheria iliyopo inataka wanaopata posho kuanzia Sh200,000 watozwe kodi
Wakati hao yakiendelea katika Ukumbi wa Bunge ulikuwa ukijaa kelele kwa wabunge kushangilia. |
No comments:
Post a Comment