Saturday, June 25, 2011

Mbunge aanguka,azirai bungeni.


 
Saturday, 25 June 2011 10:09
Kizitto Noya na Habel Chidawali, Dodoma
TAHARUKI kubwa ililikumba Bunge jana kuanzia ukumbini hadi nje baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Mwanakhamis Kassim Said (CCM) kuanguka ghafla na kuzirai.

Tukio hilo lilitokea saa 6:10 mchana wakati wabunge wakiendelea  na mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Mbunge huyo alianguka kutoka kwenye kiti chake na kisha kuzungukwa na wabunge wengi ambao walianza kumpa huduma ya kwanza. Wakati huo, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) alikuwa akichangia hotuba hiyo.

Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba kama ilivyokuwa kwa wabunge wengine wengi alionekana kushangazwa na tukio hilo.Takribani, robo ya wabunge wote waliokuwamo ukumbini humo waliinuka vitini na
kwenda kumsaidia mwenzao, kabla ya watoa huduma ya kwanza kufika na taratibu zaidi za kumpeleka hospitali mbunge huyo kufanywa.

Waandishi wa habari nao walionekana wakikimbia kwa haraka kutoka eneo lililotengwa bungeni kwa ajili yao na kutoka nje kwa lengo la kupata picha, lakini zoezi hilo liliingiwa na mushkeli baada ya askari kuwazuia.

Ndipo ukazuka ugomvi baina ya askari walikuwa wamevaa nguo za kawaida na waandishi wa habari ambao walitaka kupata picha za mbunge huyo wakati akiingizwa kwenye gari la wagonjwa na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

 Wakati askari hao wakiwazuia waandishi kupiga picha, waandishi nao walionekana kung'ang'ania ili kutekeleza kazi zao.

Hali hiyo ilizua mtafaruku mkubwa hadi Waziri Lukuvi alipoingilia kati na kuwasihi waandish hao kufuata taratibu.

 "Ndugu zangu, mkiwa humo ndani (bungeni), mko kwenye Sheria za Bunge. Sheria zingine zote zinaanza kufanya kazi mkitoa nje ya ukuta huu, ni vyema mkawasikiliza wanachowaambia,"alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi huku akiendelea kuhamasisha kutolewa kwa huduma kwa mbunge huyo.Mbali na mtafaruko, wabunge wengi zaidi walitoka nje ya ukumbi wa Bunge huku Waziri Lukuvi akiongoza harakati za kupata gari la wagonjwa (ambulance) na huduma nyingine ya kwanza kwa ajili ya mbunge huyo ambaye alionekana kupoteza fahamu.

Baadaye mchana, wakati wa akiahirisha Bunge, mwenyekiti wa kikao hicho, Mabumba alitoa tangazo rasmi kuwa mbunge huyo ameugua ghafla bungeni na amekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma."Waheshimiwa wabunge kumetokea tukio la dharura humu, mwenzetu Mwanakhamis Kasim Said, ameumwa ghafla na amepelekwa hospitali ya mkoa, taarifa zaidi zitatolewa baadaye''.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Godfrey Mtei alithibitisha kuugua kwa Mbunge huyo na kueleza kuwa anaendelea vizuri na kwamba hakuwa na tatizo kubwa.
''Ni kweli tulimpokea mbunge huyo na kweli alikuwa na hali mbaya sana wakati analetwa hapa, maana alikaa kwa zaidi ya dakika 20 akiwa hajitambui kabisa, lakini kwa juhudi za madaktari hali yake inaimarika kadri muda unavyokwenda,''alisema Dk Mtei.

Mganga huyo alisema kuwa tatizo kubwa lililogundulika katika uchunguzi wa kitabibu lilibainika kwa mbunge huyo alikuwa akisumbuliwa na uchovu mwingi uliosababishwa na kufiwa na kaka yake yake pamoja na shughuli za kibunge, hivyo alihitaji kupumzika.

Alisema wakati huo mbunge alikuwa amelazwa wodi ya daraja la kwanza hospitalini hapo, akiwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari licha ya kuwa alishaanza kujitambua na kuelewa  kilichokuwa kikiendelea tofauti na alivyofikishwa hospitalini hapo.Habari zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa mbunge huyo alikuwa akiendelea vizuri na alikuwa ameanza kujitambua pamoja na kula chakula alicholetewa.

Jumanne wiki hii, Spka wa Bunge, Anne Makinda alilitangazia Bunge kuwa mbunge huyo alikuwa Zanzibar kutokana na udhuru wa kufiwa na kaka yake.

No comments:

Post a Comment