Saturday, 25 June 2011 10:04 |
0digg Kizitto Noya, DodomaMWENYEKITI wa TLP Augustine Mrema, ametoa mpya bungeni kufuatia hatua ya kuidai serikali mafao ya kutumikia nafasi ya Naibu waziri mkuu.Akichangia mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu jana bungeni, Mrema aliitaka serikali impe mafao yake ya kutumikia nafasi ya Naibu Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili. Katika mchango wake, Mrema aliitaka serikali imlipe angalau asilimia 20, kama serikali inaona hastahili.Katika kipindi hicho, Mrema alikuwa Naibu Waziri Mkuu akimsaidia John Malecela ambaye ndiye aliyekuwa Waziri Mkuu. "Kama Sheria ipo kwamba Waziri mkuu mstaafu anatakiwa kulipwa mafao ya asimilia 80 ya mshahara wa waziri mkuu aliyeko madarakani, kwanini mimi sipati. Nipeni basi angalau asilimia 20,"alisema Mrema na kuendelea: "Nilipeni posho hiyo ili niendelee kuwatetea (serikali) bungeni. Msione simba kalowa maji mkadhani nyani. Mimi najua mambo mengi nchi hii, mmenifundisha wenyewe. Nipeni haki yangu niwasaidie kutetea hoja zetu hapa bungeni," alisema. Mrema aliendelea kuhoji imekuaje mawaziri wakuu wote wastaafu walipwe posho hiyo na yeye asipewe.Awali katika mchango wake kwenye hotua hiyo ya waziri mkuu, Mrema alitumia muda mwingi kuzungumzia umuhimu wa amani kwa Taifa akibeza maandamano ya mara kwa mara yanayoandaliwa na wanasiasa. Akitumia gazeti la Mwananchi, ambalo lilichapisha habari za athari za maandamano na ukosefu wa amani nchini Misri, Mrema alisema Tanzania itafikia hali hiyo kama wanasiasa wataendelea kuwatumia vijana kupinga serikali kwa maandamano. "Misri leo haikaliki, ndicho tunataka Tanzania, Machafuko nchini Madagascar, Libya yalianza hivyo hivyo. Ndivyo tunavyotaka Tanzania iwe, Tunisia nako machafuko tunayoyaona leo yalianzia kwenye maandamano ya kutaka kuiondoa serikali. Ndicho tunachotaka," alihoji. "Kenya nako maandamano yaliua watu 1000 na baadaye Kibaki (Mwai-Rais wa nchi hiyo) na Odinga (Laila-Waziri mkuu wa Kenya ), wakakaa huyu hapa na mwenzeke pale mezani, maisha ya watu waliokufa kwenye maandamano hayo yalimsaidia nani," aliendelea kuhoji. Mrema aliwatahadharisha wanasiasa kuacha kuandaa maandamano yasiyokuwa ya lazima na kwamba kama lengo ni kuiondoa serikali iliyoko madarakani, hilo linaweza kufanyika kwa namna mbadala. "Hawa vijana wasiokuwa na kazi tunaowahamasisha kushiriki maandamano, tukiwadekeza nchi itaingia kubaya. Ni afadhali tukawahamasisha kwenda kupiga kura kuliko maandamano, mwaka jana waliojiandikisha kupiga kura walikuwa watu 20 milioni lakini waliojitokeza kupiga kura ni milioni nane tu, hili ndilo tatizo la msingi." "Hatuwezi kuibadilisha serikali kwa hoja ya maandamano bali kwa kupiga kura. Mheshimiwa waziri mkuu nakupongeza sana katika hotuba yako unaposema amani inahatarishwa na maandamano," alihitimisha Mrema. |
No comments:
Post a Comment