Viongozi wa Somalia wamekubaliana kusitisha uhasama wa kisiasa kati yao baada ya mzozo uliodumu miezi kadhaa.
Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed na Spika wa Bunge Sheikh Sharif Aden wamekubaliana kuhairisha uchaguzi hadi mwezi Agosti mwaka ujao.
Utata huo wa viongozi umesababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya serikali ya mpito na jumuiya ya
kimataifa.Jumuiya ya kimataifa ilikuwa inashinikiza uchaguzi ufanyike Agosti mwezi huu baada ya muhula wa serikali hii ya mpito kukamilika.
Viongozi hao wametia saini muafaka wa kusitsha usahama kati yao mjini Kampala Uganda kufuatia juhudi za upatanishi zilizoongozwa na mwenyeji wao Yoweri Museveni.
Kulingana na mkataba huo, Waziri Mkuu Mohammed Abdullahi Mohammed atatakiwa kujiuzulu chini ya siku thelathini baada ya kusainiwa mkataba huo. Rais Sharif atateuwa mtu mwengine kuchukua nafasi hiyo.
Hata hivyo hatua hiyo imepingwa vikali na wafuasi wa Waziri Mkuu Mohammed, ambao wamefanya maandamano makubwa mjini Mogadishu.
Waziri Mkuu Mohammed alikuwepo mjini Kampala lakini anasemekana kuwa amerudi nchini Somalia.
Kulingana na taarifa kutoka mwakilishi wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga, viongozi wa Afrika Mashariki chini ya shirika la maendeleo la IGAD, watasimamia mkataba huo kuhakikisha unatekelezwa.
Nchi za kigeni zinazofadhili mikakati ya amani nchini Somalia, mara kadhaa zimeelezea kero zao kuhusu uhasama wa mara kwa mara wa kisiasa kati ya viongozi nchini humo.
Tofauti hizo za kisiasa ambazo wadadisi wa siasa za Somalia wanasema zinachochewa na uchu wa madaraka, zinasemekana kuchangia uzembe wa jumuiya ya kimataifa wa kuisaidia nchi hiyo kujikwamua kutoka vita vilivyo dumu miaka ishirini.
No comments:
Post a Comment