Friday, June 10, 2011

Marekani yataka Gaddafi ang'olewe haraka


Marekani imeyaomba mataifa ya Magharibi na ya Kiarabu kuongeza juhudi katika azma ya kumng'oa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.
Waziri wa mashauriano ya nchi za kigeni Bi Hillary Clinton amesema huu ndio wakati wa kumtimua Gaddafi.
Bi Clinton akihutubia mkutano wa Abu Dhabi
"Huu ni wakati wetu,mazingira yanaturuhusu.Gaddafi amefika kikomo'', Bi Clinton alisema katika mkutano wa viongozi wanaokutana mjini Abu Dhabi.

Bi Clinton pia aliwaambia wajumbe kuwa lazima juhudi zaidi zifanywe za kumbana Gaddafi na utawala wake kisiasa, kidiplomasia na
kiuchumi.
Mkutano huo wa Abu Dhabi unatarajiwa kukamilisha mipango ya kuanzisha hazina maalum ya kuwasaidia waasi wa Libya.

Waakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Marekani, Jordan, Kuwait na Qatar wanakutana ili kupanga jinsi Libya itakavyokuwa baada ya kumtimua Gaddafi uongozini.

Wakati huo huo Tripoli imekanusha madai ya uhalifu wa kivita ambayo yamewasilishwa mbele ya baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu mjini Geneva.
Baraza hilo la Umoja wa Mataifa kwa wakati huu linajadili madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu yanayodaiwa kutekelezwa na upande wa serikali pamoja na waasi.

Lakini mwanadiplomasia wa Libya Mustafa Shaban ameliambia baraza hilo kuwa upande wa serikali hauna hatia yeyote kwani ndio unaoshambuliwa.Na amelaumu vyombo vya habari, upinzani na mamluki wa kigeni kwa kukiuka haki za kibinadamu nchini Libya ikiwemo ukatili dhidi ya watu.

No comments:

Post a Comment