Monday, June 6, 2011

U-23 yaichapa Nigeria 1-0.

Monday, 06 June 2011 10:46
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya vijana U/23, Thomas Ulimwengu ( kulia) pamoja na Jamary Mnyate kushoto wakijaribu kumdhibiti beki wa Nigeria, Edet Ibok wakati wa mechi ya kimaataifa iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Sweetbert Lukonge
MSHAMBULIAJI  Thomas Ulimwengu aliibuka shujaa baada ya kuifunga bao pekee timu ya taifa ya vijana U-23 Tanzania ilipoichapa Nigeria 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ulimwengu ambaye hivi karibuni alikuwa kwenye majaribio na klabu ya Hamburg ya Ujerumani alifunga bao hilo dakika ya 83, akimalizia vizuri krosi ya Mcha Khamis aliyeingia dakika ya 70 kuchukua nafasi ya Kigi Makasi.

Pamoja na ushindi huo wa timu ya taifa ya vijana U-23 jana shukrani nyingi kwa kipa Juma Abdul kwa kuonyesha ustadi mkubwa wa kuziba pengo la Shabaan Kado aliyekuwa akidakia Taifa Stars dhidi ya Jamhuri ya Afrika Kati.

Abdul kipa bora wa mashindano ya Kili Taifa Cup alithibisha ubora wake kwa kuokoa hatari kadhaa zilizofanywa na washambuliaji wa Nigeria iliyokuwa imetawala sehemu kubwa ya mchezo huo.

Tanzania iliushangaza ulimwengu pale ilipowatoa washindi wa medali ya dhahabu wa mwaka 2000, Cameroon kwa mikwaju ya penalti kabla ya kuivaa Nigeria washindi wa dhahabu wa mwaka 1996 na fedha 2008.

Mshindi wa mechi ya marudiano watafuzu kwa ligi ndogo hapo mwezi Desemba ili kupata timu tatu zitakazofuzu kwa michezo ya Olimpiki jijini London.

Vijana wa Tanzania wanacheza mpira bila ya malengo kwa muda wote na kumfanya Thomas Ulimwengu asiwe na kazi uwanjani, huku Nigeria chini ya nahodha wao Haruna Lukuma na Jimmy Sujie wakitawala mchezo na kupoteza nafasi nyingi za kufunga.

Ighalo Odion alikosa nafasi ya kufunga dakika 65 baada ya shuti lake kudakwa na kipa Abdul pamoja na ngome yake walikuwa mashujaa kwa Tanzania.

Kocha Jamhuri Kihwelu anafanya mabadiliko kwa kumtoa Kigi Makasy aliyeoneka kuzidiwa ujanja katikati na kumwingiza Mcha Khamis aliyeleta mabadiliko kwenye sehemu ya kiungo ya Tanzania.

Dakika saba baadaye Khamis alipata mpira kutoka pembeni na kupiga krosi nzuri iliyomkuta Ulimwengu ambaye mabeki wa Nigeria walionekana kumsahau ambaye bila ya ajili alipachika bao hilo muhimu kwa tanzania kabla ya mechi ya marudiano itayofanyika nchi Nigeria.

No comments:

Post a Comment