Friday, June 10, 2011

‘Wapinzani shirikini katika maendeleo ya taifa’


 Send to a friend
Thursday, 09 June 2011 20:32
Ally Mkoreha,
 Dodoma
VYAMA vya upinzani nchini, vimeshauriwa kujenga utamaduni wa kushiriki katika mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya taifa, ukiwamo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ili kuinua uchumi na kuwaondoa wananchi katika umaskini unaowakabili.

Ushauri huo ulitolewa jana na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philipo Mpango, alipokuwa akizungumza katika semina maalumu kwa wabunge, kuhusu mpango huo unaoanza katika mwaka 2011 hadi mwaka 2016, semina hiyo ilifanyika mjini Dodoma.
"Tunaviomba vyama vya upinzani, vishiriki katika utekelezaji wa mpango huu wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu. Ni mpango ulioandaliwa kitaalamu na utasaidia katika kuinua uchumi wa nchi, tuwe kitu kimoja katika jambo hili. Vijana wetu wapewe nafasi kwa sababu ni wabunifu na wana ujuzi, wakisaidiwa, tatizo la ajira kwao litapungua," alisema Dk Mpango.

Rai hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye alisema mpango huo ni wa taifa na wala siyo wa chama chochote cha siasa na kwamba hata CCM haipaswi kuunadi. Alisema kwa kuzingatia hilo, kila mwananchi ana wajibu wa kuchangia katika utekelezaji wa mpango huo ili ulete mafanikio yanayotarajiwa.

Akizungumzia mpango huo na kuuhusisha na hali ya sasa ya
uchumi wa Tanzania, Zitto alisema: "Tatizo lililopo ni kwamba tuna uchumi unaokuwa, lakini hali ya umaskini inazidi kuwa mbaya, wataalamu wetu wa uchumi wanapaswa kuumiza vichwa ili kujua namna ya kuondokana na hali hii."

Alisema pamoja na mambo mengine, kilimo ambacho huko nyuma kilikuwa ndiyo uti wa mgongo na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa, sasa kimekuwa hakipewi kipaumbele na kuwa na mchango mdogo katika uchumi.

"Kuna haja sasa kujipanga na kuhakikisha kuwa kilimo kinapewa msukumo mkubwa kama kweli tunataka kufikia malengo ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano," alisema Zitto.Zitto alitaka serikali kuwekeza fedha za kutosha katika miradi ya kuzalisha umeme ili kuliwezesha taifa kujitosheleza kwa nishati hiyo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi.

Mbunge huyo pia alitaka kuwe na chombo maalumu cha kusimamia utekelezaji wa kila mradi wa umeme ili ukikwama kuwe na watu watakaowajibika kwa hilo."Hakuna sababu ya kuifanya miradi yote ya umeme inayokusudiwa kutekelezwa katika mpango huu, kusimamiwa na wizara, kazi hiyo ipewe NDC (Shirika la Taifa la Maendeleo), ili kama kutakuwa na mradi utakaokwama basi tuweze kuwabana kwa urahisi, ," alisema.

Kuhusu kusimamia mpango, alisema jukumu hilo liwe na Bunge na Tume ya Mipango iwe inatoa kwa chombo hicho maendeleo ya utekelezaji mara mbili kwa mwaka.Kwa upande wake Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shaa alitaka watendaji watakaothubutu kukwamisha utekelezaji wa mpango huo wasivumiliwe na badala yake, wafukuzwe kazi.Pia alitaka hatua zichukuliwe kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo mbali mbali nchini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alisema wakati umefika sasa kwa Watanzania kutenganisha siasa  na uchumi ili mpango huo uwe wa mafanikio yanayokusudiwa."Sasa tutenganishe siasa na uchumi maana sisi tumefikia mahali pa kufanya siasa katia kila jambo hata katika mambo yale ya msingi na manufaa kwa taifa na matokeo yake ni miradi mingi kukwama," alisema Mohamed.

Alisema tayari kosa limejitokeza katika Tume ya Mipango baada ya kupewa kazi ya kuratibu utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano jambo ambalo alisema linaweza kukwamisha utekelezaji.

"Bajeti ya Tume ya Mipango ni ndogo, lakini pia wataalamu wake ni wachache, haya ni makosa yanayoweza kukwamisha mpango," alisema mbunge huyo.Mohamed alitaka Watanzania wamilikishwe rasilimali za maeneo yao ili washiriki katika utekelezaji wa mpango huo na hatimaye, kunufaika nao.

"Kila mkoa uanishe rasilimali kwa ajili ya Watanzania na zile zinazopaswa kutumiwa na wawekezaji ili kuepuka migogo kama ya watu kuvamia katika migodi ya madini," alisisitiza.Mbunge wa Kibakwe, George Simbachamwene, alisema: "Katika mpango huu lazima tusema nani anasimamia miradi ili ipofika mahali mradi unakwama katika utekelezaji, tujiwe kwa kumwajibisha.

Mbunge huyo pia alilalamikia gharama kubwa na umeme na kwamba lazima zipunguzwe ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment