Friday, June 10, 2011

CCM Arusha wamkataa rasmi Chatanda


 Send to a friend
Thursday, 09 June 2011 23:18
Moses Mashalla, Arusha na Patricia Kimelemeta, Dar
WENYEVITI wa CCM kutoka wilaya za Mkoa wa Arusha, wamekutana kujadili mgogoro wa chama mkoani humo na kutoa mapendekezo manne juu ya namna ya kumaliza mgogoro huo, ikiwamo kumwondoa Katibu wa CCM wa mkoa huo, Mary Chatanda.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa, kikao hicho kilifanyika Juni Mosi mwaka huu katika Jengo la CCM, Mkoa wa Arusha na kuhudhuriwa na wenyeviti wa chama kutoka wilaya za Arusha, Arumeru, Longido, Karatu, Monduli na Ngorongoro.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wenyeviti hao walibaini kuwa Chatanda ni chanzo cha mgogoro huo, hivyo ni bora akahamishwa au kuondolewa kabisa katika nafasi hiyo ndani ya CCM.
Mapendekezo mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho na wenyeviti hao ni Chatanda kuitwa na kuonywa ili aache kutoa matamko kinyume na taratibu za chama na kutaka itafutwe njia ya haraka kurejesha amani ndani ya UVCCM mkoani humo.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na wenyeviti hao kwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama, ambayo Mwananchi ina nakala yake, hali ya kisiasa ndani ya CCM mkoani Arusha ni tete.Barua hiyo ilidai kuwa, Chatanda ni chanzo cha mgogoro mkoani humo kwa kuwa anaendesha shughuli zake kwa ubabe, dharau, majivuno na
jeuri bila kujali mtazamo wa viongozi.
“Kwa pamoja na kwa kauli moja tumegundua kwamba, chanzo cha malumbano makubwa ndani ya CCM mkoani hapa ni Katibu wa CCM Mkoa, Mary Chatanda kwa masikitiko makubwa ni mtu ambaye amejitokeza kuwa na tabia ya kuendesha shughuli za chama kwa ubabe, dharau, majivuno na kwa ujeuri mkubwa bila kujali mtazamo wa viongozi wenzake,”ilisema sehemu ya baraua hiyo.
Halikadhalika, barua hiyo imemtaja Chatanda kuwa ni mtu anayependa kuwatisha wajumbe na wanachama wa CCM kwa kuwa  yeye ni  ofisa wa usalama wa taifa, hivyo anajua mambo mengi  na watu mbalimbali humpa taarifa za kiusalama mara kwa mara.
Katika barua hiyo yenye kurasa sita, iliyosainiwa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole huku nakala yake ikipelekwa moja kwa moja kwa Rais Jakaya Kikwete, wenyeviti hao walianza kwa kumsifia Mukama kwa kuliacha suala hilo kwa uongozi wa CCM, Mkoa wa Arusha.

CCM yatuma Kamati ya Maadili
Hata hivyo, tayari CCM makao makuu walikwishatuma kamati ya maadili kwenda kuhoji viongozi wa UVCCM na Chatanda kuhusiana na sakata hilo. Taarifa ya Kamati hiyo itawasilishwa kwenye vikao vya juu vya CCM kwa maamuzi.
Taarifa zilizoandikwa na vyombo vya habari zilidai kwamba huenda kamati hiyo iliyotumwa kutoka makao makuu ikapendekeza Mwenyekiti wa UVCCM,  James Milya , afukuzwe kwenye chama kwa kumtuhumu Chatanda bila kutoa uthibitisho wa tuhuma zake.

Mwenyekiti wa Mkoa athibitisha kukutana na Mukama
Mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha, Onesmo Nangole alipotafutwa na gazeti hili kwa lengo la kuthibitisha madai hayo, alikiri juu ya barua hiyo na wao kukutana na kutoa mapendekezo hayo.
Mukama alipotafutwa  kwa njia ya simu alipokea na kusema "aah"kisha kukata simu ghafla. Hata hivyo, baadaye alituma ujumbe mfupi wa maandishi ukisema ana shughuli nyingi na kuwa angepiga simu baadaye.
 Baadaye alitafutwa tena na gazeti hili na kumwuliza mwandishi wa gazeti hili"unataka nini"na alipoelezwa juu ya barua hiyo alikata simu ghafla.
Chatanda asema  hana taarifa ya kikao
Hata hivyo, Chatanda alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema kwamba, hana taarifa na kikao hicho cha wenyeviti, kwa sababu yupo mjini Dodoma anaposhiriki Kikao cha Bunge la Bajeti.
Alisema mara nyingi amekuwa akikutana na wenyeviti hao katika vikao vyao vya CCM Mkoa kwa sababu ni wawakilishi wa chama, lakini hajawahi kukwaruzana nao wala kuzunguza lolote kuhusu mgogoro huo.
Alisema mambo yote yanayotokea yana lengo la kumchafua.
"Kuna vikao halali vya mkoa ambavyo wenyeviti hao wanashiriki, lakini hata siku moja hawajawahi kuzungumzia mgogoro huo baina yangu na UVCCM, hizo ni njama za watu wachache kunichafua,"alisema Chatanda.
Hata hivyo, alisema kuwa tangu kutokea kwa mgogoro huo, hajawahi kuitwa na kiongozi yeyote kuonywa na kwamba anaamini hana matatizo na wana-CCM hao.

No comments:

Post a Comment