Send to a friend |
Send to a friend |
Thursday, 09 June 2011 23:37 |
0digg Neville Meena, DodomaKAMBI ya Upinzani Bungeni imedai kwamba kuna upotoshaji mkubwa katika Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, huku ikidai kwamba bajeti hiyo ni ya kulipa posho na madeni. Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kambi hiyo mjini Dodoma na kusainiwa na Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe inabainisha kuwa upembuzi uliofanywa umebaini kuwapo kwa upotoshaji mkubwa wa kitakwimu na kimaudhui uliofanywa kwalengo la kuwajengea matumaini wananchi. "Kambi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na kushangazwa na hatua ya Serikali kutenga zaidi ya robo ya bajeti kulipa madeni na kulipana posho (asilimia 27), asilimia 14 kulipa madeni na asilimia 13 kulipa posho mbalimbali," ilisema taarifa hiyo. Miongoni mwa maeneo ambayo yanadaiwa kuwa na upotoshaji ni kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la umeme, ongezeko la jumla la Bajeti ya Serikali ikilinganishwa na ile ya mwaka 2010/11, posho mbalimbali, faini kwa madereva wazembe na ulipaji wa madeni ya Serikali. Hakuna mradi mpya wa umeme Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tamko la Serikali kwamba imetenga kiasi cha Sh537 bilioni kwa ajili ya kutatua tatizo la umeme, si kweli kwani kwa jumla Wizara ya Nishati na Madini, imetengewa Sh402.071 bilioni na kwamba hakuna mradi mpya wa umeme hata mmoja utakaoanzishwa. "Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi ya kawaida Sh76,953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya maendeleo zimetengwa Sh325,448,137,000. Sh325 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160 MW, 100 Dar es Salaam na 60 Mwanza,"inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alisema katika taarifa hiyo kuwa, kutokana na hali hiyo hakuna mradi mpya wa umeme unaoonekana katika bajeti hiyo na kwamba kauli ya Mkulo ililenga zaidi kuwajengea wananchi matumaini hewa na si hatua za kweli kumaliza matatizo ya umeme nchini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hakuna ongezeko lolote halisia la fedha katika bajeti ya mwaka huu, kwani kati ya Sh13.525 trilioni zilizotengwa, Sh1.901 trilioni, sawa na asilimia 14.06 ya bajeti yote ni kwa ajili ya kulipa madeni ya Taifa. "Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya kuendesha Serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zitabaki Sh11.624 trilioni ambazoni ni sawa na fedha za bajeti ya mwaka unaomalizika wa 2010/2011," alisema Zitto katika taarifa yake hiyo na kuongeza: "Kwa kuzingatia kwamba thamani ya shilingi imekuwa ikishuka, bajeti iliyotangazwa ni ya kulipa madeni". Bajeti ya posho sasa Sh987 bilioni Kuhusu hatua za kupunguza posho, kiongozi huyo alisema hakuna ukweli wa kauli hiyo kwani Serikali imetenga kiasi cha Sh987 bilioni kwa ajili ya kulipa posho mbalimbali, fedha ambazo ni sawa na asilimia 13 ya bajeti nzima. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa kutokuwapo kwa nia ya dhati ya kupunguza posho, inaonekana katika hatua za kufanya marekebisho katika sheria ya kodi sura ya 332 ili kusamehe kodi ya mapato katika posho wanazolipwa wafanyakazi wa Serikali na wanaofanya kazi katika taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye Bajeti ya Serikali. "Hii inaonyesha kuwa kauli ya kufuta au kupunguza posho ilitolewa na Serikali ili kupumbaza wananchi, lakini haina udhati,"alisema. Taarifa hiyo ilieleza kuwa bajeti imeongeza mzigo mkubwa kwa wananchi kutokana na hatua yake ya kuongeza kiwango cha faini kwa madereva wazembe kutoka Sh20,000 hadi Sh300,000, na kwamba kiasi cha Sh50,000 kilichotangazwa na Waziri Mkulo juzi kinatofautia na maelezo kwenye vitabu vya bajeti. Alisema hatua hiyo itawaathiri wananchi hasa vijana walioajiriwa ama kujiajiri katika huduma za usafiri na usafirishaji na kwamba kipengele hicho pia kinalenga kuuhadaa umma. Serikali juzi ilitangaza hatua kadhaa za kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, lakini fedha za matumizi mengineyo, maarufu kama Other Charges (OC), zimeongezwa kwa asilimia 8.62 ikilinganishwa na Bajeti ya Serikali inayofikia ukomo tarehe 30 mwezi huu. Fedha za OC katika bajeti mwaka ujao wa fedha ni Sh3.089 trilioni ikilinganishwa na kiasi cha Sh2.823 kilichotengwa katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, likiwa ni ongezeko la Sh266.599 bilioni. Fungu la fedha za OC ndilo hutumika kugharimia posho mbalimbali kwa watumishi wa umma na uendeshaji wa semina, warsha na makongamano pamoja na kugharimia safari za viongozi ndani na nje ya nchi. Kafulila adai bajeti haijazingatia vigezo vya uchumi Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliliambia Mwananchi katika viwanja vya Bunge kuwa, hali hiyo inadhihirisha kwamba bajeti iliyowasilishwa na Mkulo ililenga zaidi kutafuta kuungwa mkono kuliko kuzingatia vigezo vya kiuchumi. "Kama mwaka wa fedha unaoishia mwishoni mwa mwezi huu fedha za OC ni kidogo kuliko zile ambazo zimetengwa mwaka ujao wa fedha, basi ni dhahiri kwamba hatuwezi kusema posho zitapunguzwa, hapa nadhani kuna tatizo,"alisema Kafulila. Alisema fungu la fedha za OC lazima lipitiwe upya kwani fedha zilizotengwa ni zaidi ya kiasi cha fedha ambazo Serikali imeomba kutoka kwa nchi wahisani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. "Iwapo fedha za OC ni Sh3 trilioni na fedha za miradi ya maendeleo tunazoomba kutoka kwa wafadhili ni kiasi hicho hicho, utaona kwamba ni jambo la kushangaza, hapa kuna mambo mengi ya kuweka sawa,"alisema Kafulila, huku akibainisha kuwa bajeti hiyo ya Serikali si mbaya sana kwani imekumbuka umuhimu wa miundombinu ya usafirishaji. Akiwasilisha bungeni juzi Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12, Waziri Mkulo alibainisha hatua kadhaa za Serikali kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima akiahidi kupunguza posho zisizo na tija, safari za ndani na nje za viongozi na ukubwa wa misafara ya viongozi hao ili fedha husika ziweze kutumika kugharimia shughuli nyingine za maendeleo. "...........Serikali itasitisha ununuzi wa samani za ofisi, hususan zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyokuwa na tija, kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya Serikali, kupunguza safari za ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa misafara na kuendelea kupunguza semina na warsha, isipokuwa pale inapobidi na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu..," alisema Mkulo. Sh3 trilioni kutoka nchi wahisani Kadhalika majedwali ya ufupisho wa hesabu za bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12 yanabainisha kuwa fedha za maendeleo zinazotarajiwa kutoka kwa nchi wahisani ni kiasi cha Sh3.054 trilioni. Kiasi hicho kinazidiwa kwa asilimia 18.9 sawa na Sh5.853 bilioni kikilinganishwa na fedha za OC ambazo ni Sh3.089 trilioni. Katika bajeti hiyo, fedha zote zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh4.925 trilioni, ambapo fedha za ndani ni Sh1.871 trilioni. Mchanganuo mzima wa bajeti hiyo unaonyesha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa ni sawa na asilimia 31 ya bajeti nzima, wakati fedha za matumizi mengineyo (OC) ni sawa na asilimia 32, mishahara asilimia 23, malipo ya madeni asilimia 8, madeni mengine asilimia 3 na riba ya madeni ya ndani na nje asilimia 3. |
No comments:
Post a Comment