Friday, July 15, 2011

Mchumba wa Slaa avamiwa, aporwa.

 
Thursday, 14 July 2011 22:27

JOSEPHINE Mushumbushi, ambaye ni mchumba wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, amevamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi na kuporwa simu mbili, kamera na fedha taslimu sh 50,000.

Tukio hilo ambalo lilitokea jijini Dares Salaam juzi, karibu na SUMA-JK, ni mwendelezo wa wimbi la matukio ya uhalifu wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alifafanua kwamba tukio hilo lilitokea juzi mnamo saa 11:57 jioni, wakati Mushumbushi akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T932 ASH.

Alisema katika tukio hilo, watu hao wanne walimvamia Mushumbushi kisha kumpora mkoba wenye simu mbili aina ya Nokia, kamera 'digital' moja, nyaraka mbalimbali na fedha hizo taslimu na kuongeza, "Tunawataka wenye bodaboda kusaidia polisi vinginevyo biashara yao itapoteza heshima na kufa kwani watu watajua wote ni majambazi."

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, katika tukio hilo ambalo ni la uhalifu wa kawaida kama yalivyo matukio mengine, watu hao pia walifanikiwa kuchukua kadi tatu za benki ya CRDB, 
moja ya NMB na NBC.

Alisema watu hao walilivamia gari hilo wakati likiwa katika foleni na kuvunja kioo cha dereva kwa kutumia nyundo kisha kupiga risasi hewani, hali iliyomshtua Mushumbushi ambaye ni mjazito.

Kamanda Kenyela alisema baada ya Polisi wa Oysterbay kupata taarifa hizo, walifika eneo la tukio kisha kutoa msaada wa kutoa gari ambalo liliingia kwenye mtaro kisha kumsaidia mama huyo kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala.

 "Unajua alipata mshtuko kwasababu ni mjazito. Baada ya kupata taarifa hizo askari waliwahi eneo la tukio kisha kumsaidia kutoa gari kwenye mtaro na kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala. Baadaye aliruhisiwa na mimi nilionana naye saa 4:00 usiku," alifafanua Kamanda Kenyela.

Alisema muda huo, Dk Slaa na mama alifika Polisi Oysterbay akiwa na mchumba wake huyo kwa ajili ya kuandikisha maelezo, na kisha kusindikizwa kupelekwa nyumbani na hadi sasa hali yake ni nzuri.

Kuhusu watuhumiwa, alisema tayari juzi hiyo walifanikiwa kupata mkoba huo ukiwa na baadhi ya vitu isipokuwa simu, fedha na kamera huku akihiadi, "napenda kuhakikishia public (umma), polisi itawakamata watuhumiwa wote."
venance.chadema@yahoo.com

No comments:

Post a Comment