Send to a friend |
Thursday, 14 July 2011 22:25 |
JUMLA ya washtakiwa 31 kati ya 36 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Kiuchumi wa Tanzania maarufu kama kesi ya samaki wa Magufuli wameachiwa huru. Washtakiwa hao kutoka Mataifa ya China, Ufilipino, Vietnam na Kenya walikuwa wakituhumiwa kufanya shughuli za uvuvi katika eneo hilo bila kuwa na kibali na kuchafua mazingira ya bahari katika eneo hilo. Lakini jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaa mbele ya Jaji Augustine Mwarija anayesikiliza kesi hiyo iliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kuridhika kuwa hawana kesi ya kujibu kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili. Wakati wakiachiwa huru jana washtakiwa hao walikuwa wameshasota mahabusu kwa muda wa miaka miwili na miezi minne tangu walipokamatwa Machi 9 hadi walipoachiwa huru jana.Wakati 31 wakiachiwa huru kwa kutokuwa na kesi ya kujibu washtakaiwa wengine watano wamepatikana na kesi ya kujibu na hivyo mahakama kuwataka wajitetee kuhusiana na tuhuma hizo. Waliopatikana na kesi ya kujibu ni pamoja na mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Hsu Chin Tai ambaye ni Nahodha wa meli waliyokuwa wakiitumia kwa shughuli za uvuvi. Wengine ni mshtakiwa wa saba Zhao Hanquing, mshtakiwa wa tisa Hsu Sheng Pao ambao wote ni mawakala wa meli hiyo, pamoja na wahandisi wawili wa meli hiyo Cai Dong Li mshtakiwa wa 33 na Chen Rui Hai mshtakiwa wa 34. Akisoma uamuzi wake jana Jaji Mwarija alisema kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka hususani ushahidi wa shahidi wa tatu Nahodha Ernest Bupamba kutoka Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi ameridhika kuwa washtakiwa hao wana kesi ya kujibu. Bupamba ambaye ni Ofisa msimamizi wa sheria na shughuli za uvuvi katika ushahidi wake aliieleza mahakama kuwa ndiye aliyewakamata wakati wakifanya doria na timu ya wanadoria kutoka mataifa matatu. Mbali na ushahidi wake wa mdomo kuwa rada aliposoma kwenye rada iliyokuwa kwenye meli yao ya doria ilionyesha kuwa walikuwa katika eneo la Tanzania, pia Nahodha Bupamba aliwasilisha mahakamani vielelezo huku akiwasilisha mahakamani vilelezo vya picha zinazohusiana na mashtaka hayo. Tai (nahodha), Li na Hai (wahandisi) wakipatikana na kesi ya kujibu katika kosa la kwanza la kufanya shughuli za uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu ya Tanzania bila kuwa leseni na kosa la pili la kuchafua mazingira ya bahari kwa uchafu wa samaki na mafuta ya meli. Kwa upande wao Hanquine na Pao (mawakala) wao walipatikana na kesi ya kujibu katika kosa la tatu ambalo ni kosa mbadala wa kosa la kwanza na la pili, yaani kosa la kutaka kuwasaidia washtakiwa wengine wakwepe mashtaka(Accessory after the fact). Katika shtaka hilo la tatu washtakiwa hao wanatuhumiwa kuwa baada ya washtakiwa wengine kukamatwa washtakiwa hao walifika nchini wakiwa na leseni na hati za meli ili kuonyesha kuwa walikuwa wakifanya shughuli za uvuvi kihali ili wapone katika mashtaka hayo. Kabla ya kuwaachia hao 31 na kuwakuta na kesi ya kujibu watano kwanza Jaji Mwarija alianza kwa kurejea majumuisho ya hoja za pande zote na kuanza kuchambua moja baada ya nyingine, huku akitupilia mbali na kukubaliana na baadhi ya hoja za pande hizo zote. Baada ya kufanya uchambuzi wa hoja hizo Jaji Mwarija alisema kuwa ameridhika kuwa kwa jinsi inavyoonekana kutokana na ushahidi uliopo upande wa mashtaka umethibitisha kesi katika shtaka la kwanza na pili. “Lakini swali la kujiuliza ni kwamba ni kwa nani upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi katika makosa hayo,” alijihoji Jaji Mwarija.Alisema hakubaliani na upande wa mashtaka kuwa umethibitisha kesi katika mashtaka hayo kwa kila mshtakiwa. Aliongeza kuwa ushahidi wa washtakwa wote kukutwa tu ndani ya meli hautoshi kwani majukumu ya kila mmoja katika meli hayakuwekwa wazi na kwamba upande wa mashtaka ulipaswa kuliweka wazi, kwani si kweli kwamba wote walikuwa wakivua samaki. “Kigezo katika shtaka la kwanza ni kuvua bila kuwa na leseni. Lakini kuna ushahidi kwamba wengine walikuwa ni wapishi ndani ya meli ile,” alisema Jaji Mwarija na kuongeza kuwa kwa mujibu wa shahidi wa sita (PW6) suala la leseni ni jukumu la nahodha. |
No comments:
Post a Comment