Thursday, 14 July 2011 22:19 |
Kiungo wa Simba, Mohamed Banka (Kushoto) akiwa amejishika kiuno kwa huzuni asiamini kilichotokea akiwa na kocha Moses Basena (katikati)na Kelvin Yondani (kulia) aliyeinamisha kichwa baada ya kumalizika pambano lao dhidi ya Simba na kufungwa na Yanga bao 1-0 katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame. Picha na Jackson Odoyo.
WINGA wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba, Uhuru Selemani amewasihi mashabiki na viongozi wa timu hiyo kuacha tabia ya kuwahukumu wachezaji kwamba walihujumu na kufungwa na wapinzani wao Yanga bao 1-0 kwenye fainali ya Kombe la Kagame iliyofanyika Jumapili iliyopita kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kauli ya nyota huyo ambaye hivi karibuni amerejea dimbani baada ya kupona goti lililokuwa linamsumbua inafuatia kitendo cha baadhi ya mashabiki wa Simba kuwatuhumu baadhi ya wachezaji kuwa ndio sababu ya timu yao kufungwa na Yanga siku ya fainali.
Wachezaji wa Simba wanaoshutumiwa na mashabiki kuwa walifanya hujuma na kuchangia timu hiyo kufanya vibaya ni kiungo Mohamed Banka, mshambuliaji Musa Hassan Mgosi na beki Kelvin Yondani.
Simba ilikuwa haipewi hata nafasi ya kufika kwenye raundi ya pili kutokana na kuwa na kikosi dhaifu baada ya kutimua nyota wake wengi siku chake kabla ya michuano hiyo, lakini wachezaji hao waliweza kupigana na kufika fainali.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana Uhuru alisema kitendo cha kuwahukumu wachezaji katika mchezo mmoja tu kinaonyesha jinsi gani mashabiki wa timu hiyo hawana uvumilivu na kusahau mazuri yaliyofanywa na wanaowatuhumu katika siku za nyuma.
"Mpira hauko hivyo mashabiki wanatakiwa waelewe hauwezi kucheza vizuri siku zote, kuwalaumu wachezaji fulani sio sahihi na hii inaonyesha ni jinsi gani tunavyokosa uvumilivu na kusahau mazuri yaliyofanywa na hawa hawa tunaowalaumu."
"Kwa mfano Mgosi mimi namjua vizuri sana na yeye ananifahamu, nina uhakika tukianza kucheza pamoja atafunga mabao mengi, wewe subiri ligi ianze," alisema Uhuru.
Selemani pia aliwaasa viongozi kuacha fikra za kuwafukuza wachezaji kutokana na matokeo yao na Yanga na badala yake waimarishe kikosi ili kiweze kufanya vizuri msimu ujao.
"Sawa inawezekana labda kuna ambao viwango vyao vimeshuka, lakini hili la kumwacha mchezaji kwa sababu ya matokeo ya mechi ya Simba na Yanga sio sahihi, hapa watatakiwa kutafakari kwa makini na pia ni vizuri kuimarisha timu ili iweze kufanya vizuri msimu ujao,"alisema Uhuru.
Akizungumzia sakata la kutaka kuachwa na Simba kiungo Banka, alilimbia gazeti hili kwa simu yake ya mkononi , "mimi sina taarifa rasmi zinazohusiana na kutemwa na klabu hiyo zaidi ya kusoma na kusikia kupitia vyombo vya habari kama watu wengine."
"Sina cha kuongea ndugu yangu kuhusu hilo kwa sababu sina taarifa rasmi za kiofisi, hebu ngoja tusubiri tuone kitakachotokea,"alimaliza Banka ambaye alicheza mechi zote za Simba kwenye kikosi cha kwanza kwenye mashindano ya Kagame, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho msimu huu.
Imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wa Simba na Yanga kuwashutumu wachezaji wao kwamba wamehongwa au kuhujumu mechi kila timu hizo zinapocheza na moja kufungwa, hakuna upande huwa unakubali matokeo hayo yalikuwa ya uwanjani. |
venance.chadema@yahoo.com
No comments:
Post a Comment