Wednesday, August 24, 2011

Gaddafi, waasi ngoma nzito

venance.chadema@yahoo.com

 
Tuesday, 23 August 2011 20:39

WAASI wa Libya wanaosaidiwa na Vikosi vya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO), wamedai kwamba wameyateka makazi ya Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi katika Mji Mkuu wa Tripoli.
Juzi usiku, waasi hao walitangaza kuingia Tripoli ambako ni ngome muhimu ya Gaddafi na vikosi vyake lakini hadi jana, licha ya kiongozi huyo kutojulikana aliko huku watoto wake wa tatu waliodaiwa kukamatwa na waasi hao wakionekana mitaani, hakuna upande uliokuwa umetangaza udhibiti wa moja kwa moja wa mji huo.

Katika siku hiyo ya pili ya mapambano, majeshi ya Gaddafi yamedaiwa kutumia silaha nzito wakati waasi nao wakijitangazia kusonga mbele ili kuishikilia Tripoli nzima baada ya
kushikilia baadhi ya maeneo.

Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera, James Bays alisema jana kuwa mapigano hayajaisha na jiji la Tripoli lipo katika hali tete kiusalama.

Waasi wadai kuingia katika makazi ya Gaddafi
Bays alisema waasi walifanikiwa kuingia katika makazi ya Gaddafi kupitia moja ya milango iliyopo katika majengo yake huku mapambano makali yakiendelea baada ya majeshi ya kiongozi huyo kukabiliana vikali na waasi hao.

Hata hivyo, hakukuwa na upande wa pili wa taarifa kutoka kwa Serikali ya Gaddafi kuthibitisha ukweli au uongo wa madai hayo ya waasi ambao juzi walitamba kuwakamata watoto watatu wa kiongozi huyo, lakini baadaye ikabainika ilikuwa ni propaganda za kivita.

Waasi hao walidai kuwa wamemkamata mtoto wa Gaddafi anayejulikana kwa jina la Saif al-Islam lakini jana asubuhi alijitokeza kwenye Mji wa al-Mansoura, kitendo kilichozua maswali mengi baada ya waasi kudai kuwa wanamshikilia na kwamba wameidhibiti Tripoli.

Pia, kiongozi wa Baraza la Mpito la Libya (NTC), alitangaza kuwa mwisho wa uongozi wa muda mrefu wa Gaddafi umefika baada ya kudai waasi wanaishikilia Tripoli.

Hata hivyo, pamoja na kwamba waasi hao wako Tripoli lakini hadi jana wameshindwa kufahamu aliko Kanali Gaddafi na wamekuwa wakitoa taarifa za kubashiri.

Taarifa kuhusu Gaddafi
Kiongozi huyo kwa mara ya mwisho alisikika Agosti 21, mwaka huu baada ya kuwataka wananchi wote wa Libya kuungana naye katika mapambano dhidi ya waasi na Nato.

"Niko Tripoli," aliliambia shirika la habari la Libya kwa njia ya simu na kuongeza, "Tokeni nje mkapambane, niko pamoja nanyi mpaka mwisho,"aliwaambia watu wake, lakini hajawahi kuonekana mbele za watu tangu Mei mwaka huu lakini hadi jana alikuwa akidhaniwa kujificha mjini Bab al Aziziyah.

Lakini, taarifa ambazo hazijathibitishwa rasmi na mamlaka yoyote zinaeleza kwamba Gaddafi ameondoka Tripoli kuelekea eneo alikozaliwa katika Mji wa Sirte, Magharibi mwa Libya, kwa kupita kwenye barabara iliyoko chini katika makazi yake.

Katika hatua nyingine, Saif ambaye juzi alitangazwa na waasi kwamba alikamatwa, jana aliibuka na kuzungumza na waandishi wa habari wa kimataifa katika Hoteli ya Rixos na kusema Tripoli ilikuwa bado mikononi mwa Serikali ya  Libya iliyo chini ya baba yake.

Mmoja wa viongozi wa NTC, Waheed Burshan alisema: “Tulikuwa na uhakika kuwa Saif al-Islam alikuwa amekamatwa lakini hatuelewi ametoroka vipi.”

NTC ilifanya mkutano wa waandishi wa habari jijini Benghazi wakiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

"Tunasimama upande wa kiongozi wa NTC, Mustafa Abdel Jalil kwa kuwa ameweza kufikisha waasi Tripoli kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya Libya," alisema Davutoglu.

Madaktari waomba dawa zaidi za binadamu
Madaktari wameomba kusambazwa kwa dawa zaidi na kuongezewa nguvukazi kutokana na kuongezeka kwa majeruhi wengi wanaotokana na mapambano yanayoendelea.

Dk Bousnina aliliambia Shirika la Habari la Sky la Uingereza kwamba wanahitajika madaktari wa nyongeza, pia watu watakaojitolea damu na wasaidizi wa kawaida ili kukabiliana na hali ilivyo nchini humo.

"Nawaombeni watu wa Libya ambao mnanisikiliza muda huu, mje mjitolee damu, pia tupate watu watakaotusaidia kusafisha hospitali kwa kuwa hali ni mbaya," alisema.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, limekuwa likifanya usambazaji wa dawa na kutoa matibabu kwa wagonjwa na majeruhi wa mapigano yanayoendelea.

Uingereza yazungumza
Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Nick Clegg amesema kuwa ni suala la muda tu kwa uongozi wa Kanali Gaddafi kushindwa na waasi.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Uingereza, Clegg ilisema kujitokeza kwa mtoto wa Kanali Gaddafi, Saif Al-Islam hakumaanishi kuwa uongozi wa Gaddafi unarudi.

"Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa majeshi ya kuikomboa Libya yameukamata Tripoli lakini si yote," alisema.

"Ndiyo kutakuwa na kuchanganyikiwa na matatizo lakini kilichobaki katika uongozi wa Gaddafi tayari kimeshazungukwa. Ni suala la muda tu kabla ya kutangazwa rasmi kushindwa kwa Gaddafi na kuitangaza Libya kuwa iko huru."

No comments:

Post a Comment