Wednesday, August 24, 2011

Yanga kwa Moro, Simba, Coastal hapatoshi


 
Tuesday, 23 August 2011 21:09

Kocha wa Mkuu wa klabu ya Yanga, Sam Timbe

BAADA ya kushuhudia moto mkali ukiwaka kwenye ufunguzi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kitimtim hicho kinaendelea tena leo kwa timu 12 kushuka dimbani kumenyana kwenye viwanja sita tofauti.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga ikitoka kwenye majeraha ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kwenye mechi ya ufunguzi watakuwa na kazi ya kurudisha matumaini ya mashabiki wao wakati watakapoivaa Moro United.

Katika mchezo huo, Yanga ambayo imepoteza imani ya mashabiki wake baada ya kupoteza mechi tano mfululizo tangu Julai 21 inatarajia kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Moro United ambayo ilionyesha upinzani mkali kwenye mechi dhidi ya Azam FC licha ya kulazwa bao 1-0.

Kwa upande mwingine wapinzani wa Yanga, Simba SC wenyewe watakuwa kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga kukabiliana na wenyeji Coastal Union maarufu kama 'Wagosi wa Kaya'.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu hasa ukizingatia uimara wa Simba kwa sasa wakiwa wameichapa Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii  na pia kuichapa JKT Oljoro kwa idadi hiyo hiyo ya magoli.

Coastal wataweka kando undugu wao na Simba leo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, ili kijihakikishia muelekeo mzuri katika Ligi Kuu ya msimu huu.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, timu ya maafande wa Polisi Dodoma ambayo ililazimishwa suluhu na African Lyon katika mechi ya ufunguzi ,safari hii itakawakaribisha wenzao wa JKT Ruvu huku Villa Squad ikisafiri hadi mjini Bukoba kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba mjini humo.

Nayo JKT Oljoro baada ya kukaribishwa Ligi Kuu kwa kulazwa mabao 2-0 na Simba itarudi kwenye Uwanja wake wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kuikabiri Mtibwa Sugar wakati Toto African iliyoanza kampeni kwa kuitungua Villa Squad mabao 3-0 itakuwa kwenye dimba la Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kupepetana na Ruvu Shooting.

MAKOCHA WAJIGAMBA

Kocha wa Mkuu wa klabu ya Yanga, Sam Timbe amesema maandalizi kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Moro United yamekamilika baada ya timu hiyo kufanya mazoezi ya nguvu kwa siku mbili.

Timbe alisema yeye amemaliza kazi yake anachosubiri ni vijana wake kuyafanyia kazi maelekezo aliyowapa ili katika mchezo huo waibuke na pointi tatu.

“Nimekuwa nikinoa sana safu ya ushambuliaji katika mazoezi yangu hii inatokana na safu ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi za kufunga katika mchezo na JKT hivyo nataka hali ile isijitokeze tena katika mchezo wetu wa leo na hawa Moro United ila nina imani tutapata ushindi mzuri tusubiri dakika 90.”

Timbe pia aliwataka mashabiki kuwa watulivu timu yao inapofanya vibaya kwani hali hiyo hakuna anayeipenda itokee isipokuwa ni hali ya kimchezo.

"Mashabiki wanapaswa kujua njia ya kutatua matatizo kwa amani tofauti na mbinu zinazofanyika hivi sasa za kutoa shutuma kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa kutoa kauli za vitisho, kufanya hivyo wanakosea," alisema Timbe.

Jijini Tanga; Kocha wa Simba, Moses Basena alisema timu yake imewasili Tanga ikiwa haina tatizo kwa sababu ina majeruhi mmoja tu Mwinyi Kazimoto na kwamba ipo tayari kukwaana na Coastal Union.

“Nashukuru Mungu timu yangu wachezaji wote wako fiti tuna majeruhi mmoja tu Mwinyi Kazimoto, tuko tayari kwa mechi na Coastal," alisema Basena.

Mashabiki wa Simba waliojitokeza katika mazoezi hayo walisema ushindi wa mchezo wa fungua dimba uliwapa matumaini na wanaamini kwamba wataifunga Coastal leo.

Naye Kocha wa Coastal Union, Hafidh Badru alisema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo baina yao na Simba na kwamba wana uhakika wa kuifunga kwani makosa yaliyofanyika walipocheza na Mtibwa Sugar yamesahihishwa.

“Dosari zilizotokea katika mchezo tuliocheza na Mtibwa tukatoka sare ya bao 1-1 tumeshazirekebisha hivyo wapenzi wa Coastal Union wategemee ushindi leo, hatoki mtu Mkwakwani,”alisema Badru.

Mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union, Ahmed Aurora aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani Mkwakwani leo ili kuipa nguvu na kuishangilia timu yao katika pambano lake na Simba.

Baada ya mechi hizo za leo, ligi itasimama kwa muda ili kupisha maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, ambapo Taifa Stars itacheza na Algeria Septemba 3.

Ligi itarejea tena Agosti 27 kwa mchezo mmoja utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi kati ya African Lyon itakayokuwa mwenyeji wa Toto African kutoka jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment