venance.chadema@yahoo.com
Tuesday, 23 August 2011 20:24 |
CHUO Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), kimevumbua chanjo inayotibu magonjwa mbalimbali kwa kuku na wanyama wengine iliyotokana na mimea nchini. Mratibu wa Haki Miliki wa Sua, Profesa Amini Kweka, alisema chanjo hiyo imevumbuliwa na wataalamu wa chuo hicho na kutengenezwa chuoni hapo. Profesa Kweka alisema tayari wameifanyia majaribio nchi nzima na imeonyesha mafanikio makubwa kuliko dawa zingine zilizoko madukani.
“Chanjo hii inatibu magonjwa mengi ya kuku na wanyama wengine, baada ya
majaribio tumegundua ni bora kuliko hata zile zilizoko madukani,” alisema Profesa Kweka. Alisema hivi sasa wako kwenye majadiliano na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ili waweze kuruhusu ianze kutumika. Alisema kuvumbuliwa kwa chanjo hiyo kutapunguza gharama kwa sababu imetengenezwa kwa rasilimali zilizopo nchini.
Pia, Profesa Kweka alisema chuo hicho kimeweka sera ambayo bidhaa zote zitakazogunduliwa na ambazo zitakuwa zimetumia rasilimali za nchi na chuo, ziandikishwe. Alisema walifikia hatua hiyo baada ya bidhaa zingine zilizovumbuliwa na chuo hicho, kuchukuliwa na kampuni za nje kutokana na kutowekwa haki miliki.
Alisema baadhi ya bidhaa hizo ni dawa za mifugo na trekta lililotengenezwa na Profesa Makungu kutoka chuoni hapo, ambalo limeonekana kumilikiwa na kampuni nyingine wakati ni mali ya Sua.
“Hata kwa watafiti wanaokuja nchini wanaotumia rasilimali za chuo, wanatakiwa wawe na mkataba maalumu na chuo kuhakikisha chochote watakachoona kinatambuliwa na chuo na nchi,” alisema. Profesa Kweka alisema hivi sasa wanaendelea na mradi mwingine wa kuimarisha matumizi ya ubunifu katika kilimo na maliasili, ambao unatumia wataalamu wa chuo kutatua matatizo ya viwanda vilivyoko nchini. Edited by Midraji Ibrahim |
No comments:
Post a Comment