Tuesday, August 9, 2011

Uchunguzi tuhuma za Jairo ngoma nzito

venance.chadema@yahoo.com


Monday, 08 August 2011 21:30
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, unaendelea na siku kumi zilizotolewa hazitoshi.

Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, akizungumzia hatua za haraka za Serikali kushughulikia kashfa hiyo, ilisema uchunguzi huo dhidi ya Jairo ungetumia siku 10, lakini Julai 31, ambayo ilikuwa ni siku ya kumi, CAG Utouh alisema ndiyo kwanza alikuwa na siku ya tano tangu kuanza ukaguzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Utouh alisema uchunguzi siyo kuandika ripoti, kwani
kuna mambo mengi ya msingi ya kitaalamu yanapaswa kuzingatiwa.
Kwa mujibu wa Utouh, dhamira ya Ikulu na ofisi yake ni kuhakikisha uchunguzi unaofanyika unatoa matokeo mazuri, ambayo yataonyesha undani wa tuhuma zenyewe na suala siyo kuandika ripoti kama inavyoweza kufikirika na baadhi ya watu.
 
"Muda is not an issue (muda siyo hoja), jambo la msingi ni kufanya uchunguzi utakaoleta tija kwa kile kilichokusudiwa. Siyo kwamba tunakaa na kuandika ripoti tu, tunafanya uchunguzi wa kina kupata majibu ya msingi ambayo Watanzania wataona matokeo ya uchunguzi wetu," alisema Utouh.
Utouh alisema katika uchunguzi huo kuna kupitia nyaraka mbalimbali za msingi na kwamba, licha ya nyaraka, wanahitaji kufanya mahojiano na watu mbalimbali waliotuhumiwa.

Hata hivyo, CAG alisema uchunguzi huo kwa sasa uko hatua za mwisho, lakini alipoulizwa ni lini unaweza ukawa umekamilika rasmi alijibu: "Hilo siwezi kukwambia."

"Unachopaswa kujua ni kwamba uchunguzi uko hatua za mwisho, sasa kukwambia ni lini siwezi. Jua tu tunakamilisha kazi na jambo la msingi tuje na matokeo mazuri. hivi ninavyokwambia (jana) hapa nipo ofisini ingawa leo ni Nanenane,” alisema na kuongeza:
“Leo ni sikukuu ya Nanenane, lakini kuna kazi zingefanyika nje, nyingine tunazifanya hapa hakuna kupumzika licha ya kwamba ni sikukuu. Ni kwa sababu ya jambo hilo."

Kauli ya Ikulu kupitia Luhanjo
Julai 21, Luhanjo alitangaza uchunguzi huo ambao ulionekana ni hatua za haraka za serikali kushughulikia tatizo hilo, ambalo liligusa hisia za wabunge na watu wa kada mbalimbali nchini, wakiwamo viongozi wa dini.

"Nimeanzisha uchunguzi wa awali (Preliminary Investigation) kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo. Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, amepewa likizo ya malipo kupisha uchunguzi wa awali (Relieve of duties administratively pending preriminary investigation)... hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye zitategemea matokeo ya uchunguzi huo," alisema Luhanjo.

Luhanjo alisema ikiwa uchunguzi wa CAG utabaini Jairo ana makosa ya nidhamu, atapewa taarifa za tuhuma husika (Notice) ambayo itaambatana na hati ya mashtaka (charge), ambayo itaeleza kwa kifupi makosa hayo na jinsi yalivyotendekea.

No comments:

Post a Comment