Tuesday, August 9, 2011

Madiwani waliotimuliwa Chadema wajipanga kwenda mahakamani .

venance.chadema@yahoo.com


Monday, 08 August 2011 21:28

KUNA uwezekano wa madiwani watano wa Chadema, waliovuliwa uanachama na kamati kuu ya chama hicho mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo.

Uwezekano huo ulielezwa na Diwani wa Kata ya Elerai, John Bayo,
alipozungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kutokea Dodoma walipokwenda kuhojiwa kabla ya uamuzi wa kutimuliwa kufikiwa.
“Binafsi sina kinyongo na chama changu wala viongozi wake. Nimepokea uamuzi huo kwani ndiyo msimamo wa vikao, lakini nakuhakikishia bado nina imani ya kuendelea na nafasi yangu ya udiwani hadi uchaguzi mkuu ujao, kuna njia nyingine ya kupinga uamuzi huo kupitia vikao au
mahakamani,” alisema Bayo.

Bayo alisema kabla ya kuchukua uamuzi wowote watazungumza na wapiga kura kwenye kata zao, kuwaeleza yaliyojiri na kuacha nafasi ya uamuzi wa hatua zinazostahili mikononi mwa umma uliowaamini na kuwapa dhamana ya uongozi.
“Pia, tutawasiliana na wanasheria wetu kuangalia mwanya wa hatua za kisheria kama zipo, ili kulinda na kutetea haki zetu za msingi iwapo zitagundulika kukiukwa katika uamuzi huo,” alisema.

Bayo aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Madiwani wa Chadema Manispaa ya Arusha, alitimuliwa kwa kugoma kujiuzulu wadhifa wa uenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi aliopata kutokana na mwafaka waliofikia kati yao na wenzao wa TLP na CCM.

Wengine waliotimuliwa na kata zao kwenye mabano ni, Estomih Mallah (Kimandolu), Charles Mpanda (Kaloleni), Reuben Ngowi (Themi) na Rehema Mohamed wa Viti Maalumu. Diwani wa Kata ya Sekei, Chrispine Tarimo, uamuzi wake umewekwa kando baada ya kutohudhuria kikao cha Dodoma kutokana na udhuru.
Kuhusu iwapo watajiunga na vyama vingine vya siasa kuomba uteuzi wa kutetea udiwani, Bayo alisema wanasubiri uamuzi wa wananchi kufikia hatima yao kisiasa.

Wakati hayo yakitokea, wananchi 48 kati ya 50 waliohojiwa jana kuhusu uamuzi wa kutimuliwa kwa madiwan hao waliunga mkono wakisisitiza kutochukua hatua hiyo kungefanya chama hicho kukosa nguvu ya kukinyooshea kidole CCM kwamba inashindwa kufanya uamuzi mgumu.
“Kamati kuu ni kikao cha juu kwa uamuzi katika chama chochote cha siasa, kikitoa agizo na likapuuzwa na mwanachama au kiongozi yeyote, halafu chama kisichukue hatua ingekuwa ni udhaifu. Hata hawa madiwani walijua adhabu yao ni kufukuzwa, hivyo wamepata stahili yao,” alisema Karim Abdalah, mkazi wa Kaloleni.

Karim aliyejitambulisha kuwa mkereketwa wa CCM, alisema uamuzi wa kuwadhibiti wanaokiuka maadili na maelekezo ya vikao vya uamuzi, ni utamaduni uliozoeleka katika chama chake inayowadhibiti wote wanaokiuka maagizo na maelekezo ya vikao halali.

Kwa upande wake, John Meddah, mkazi wa Sekei na mwanachama wa CCM yeye alipinga uamuzi huo licha ya kukiri kuwa, hata chama chake kiliwahi kuwatimua udiwani madiwani wawili wa Manispaa ya Arusha, Mussa Mkanga (Sombetini) na Mary Kisaka (Viti Maalumu), huku aliyekuwa meya Paul Lota Laizer akivuliwa wadhifa wake.

No comments:

Post a Comment