venance.chadema@yahoo.com
Mtoto aliyeibwa Bunda miaka saba iliyopita apatikana nchini Kenya |
|
Sunday, 07 August 2011 21:50 |
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mtoto aliyeibwa wilayani Bunda, mkoani Mara miaka saba iliyopita, amepatikana nchini Kenya, baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa amemwiba kuugua na kufariki dunia.
Mtoto huyo wa kiume Nyambibiti Lazaro, ambaye sasa hajui lugha yoyote tofauti na kijaluo, aliibwa na mwanamke wakati huo akiwa na umri wa miezi minne, wakati mama yake mzazi alipokuwa amemwacha nyumbani kwao, akiwa chini ya uangalizi wa mtoto mwenzake mwenye umri wa miaka mitano.
Polisi wilayani hapa wamesema kuwa siku ya tukio mwanamke mmoja alifika nyumbani hapo na kuomba maji ya kunywa na kisha akamlaghai mtoto huyo kuwa amepewa fedha na mama yake ya kununulia mboga sokoni na hivyo waambatane naye kwenda sokoni.
Ilielezwa kuwa baada ya kufika katika nyumba moja ya kulala wageni iliyoko mjini Bunda, alikokuwa amefikia mwanamke huyo, alimpatia Sh 500 mtoto huyo na kumwambia kuwa aende sokoni anunue samaki na kwamba yeye atamsubiri na mtoto huyo katika eneo hilo.
Aidha, ilielezwa kuwa baada ya mtoto huyo kuondoka, mwanamke huyo aliingia ndani ya chumba chake na kumwambia mhudumu kuwa alikuwa amefuata mtoto wa ndugu yake hospitalini na kisha akabadili nguo na kutokomea na mtoto huyo kusikojulikana.
Mzazi wa mtoto huyo, Lazaro Kamuli, alisema kuwa alifuatilia kila sehemu na hakuweza kumpata mtoto wake na akaamua kukata tamaa huku yeye na familia yake wakiendelea kumwomba mwenyezi Mungu na kwamba kupatikana kwa mtoto wake nchini Kenya, kumechangiwa na vyombo vya habari kuripoti tukio hilo baada ya kuwa limetokea.
Alibainisha kuwa Julai 24 mwaka huu, alipigiwa siku kwamba mtoto wake amepatikana katika kijiji kimoja nchini Kenya na kwamba mwanamke aliyekuwa amemwiba alifariki dunia na sasa mtoto huyo yuko chini ya uangalizi wa Serikali ya Kenya.
Ilielezwa kuwa awali mwanamke huyo alikuwa ameolewa na mwanamume mmoja katika Kijiji cha Manira-Shirati, wilayani Rorya na walitengana na mwanamume huyo miaka mitatu kabla ya kukimbilia nchini Kenya.
Alisema alichukua vielelezo vyote kutoka Jeshi la Polisi na kwenda huko nchini Kenya na kwamba baada ya kufika katika mji alikokuwa anaishi mtoto huyo, wenyeji wake walimwambia kuwa ili aweze kupewa mtoto huyo bila usumbufu wowote, ajifanye kuwa yeye ni shemeji wa mwanamke aliyefariki na hivyo amekuja kuchukuwa mtoto huyo kwa ajili ya kwenda kumlea.
Aliongeza kuwa alikubaliana na masharti hayo na kwamba baada ya mtoto huyo kuletwa mbele yake ghafula alimkimbilia na kumkumbatia hali ambayo iliwashangaza watu waliokuwa hapo.
‘Baada ya mtoto wangu kuletwa mbele yangu ghafla alinikimbia na kuning’angania na hiyo inaonyesha jinsi damu ya mtu isivyopotea, kitendo hicho kiliwashangaza watu wote waliokuwa katika eneo hilo," alisema.
Alisema kuwa alikabidhiwa mtoto huyo na kurejea wilayani hapa na kutoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha wilayani hapa kwa uthibitisho zaidi, ambapo Jeshi la Polisi limethibitisha kurejeshwa kwa mtoto huyo, ambaye sasa na umri wa miaka saba.
Hata hivyo alisema kuwa kutokana na damu kuwa nzito mtoto huyo baada ya kufika nyumbani kwao alicheza vizuri na watoto wanzake, licha ya kwamba anajua lugha moja tu ya kijaluo. |
No comments:
Post a Comment