Tuesday, August 9, 2011

Viongozi CUF wanusurika ajalini

venance.chadema@yahoo.com

Monday, 08 August 2011 21:27

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro na abiria wengine watano waliokuwa wakisafiri kutoka Igunga walikofanya maandalizi ya uchaguzi mdogo kuelekea Dar es Salaam wamenusurika kifo katika ajali mbaya ya gari.

Ajali hiyo ilitokea jana jioni kilomita karibu  10 kutoka mjini Morogoro barabara ya kuelekea Dar es Salaam na kumsababishia majeraha kiongozi huyo na abiria wake.

Akizungumza na Mwananchi jana jioni katika eneo la ajali Mtatiro alisema kuwa gari waliyokuwa nayo aina ya Toyota Land Cruiser lilikatika ‘stadi’ za tairi moja la mbele na kusababisha gari hilo kuyumba na kukosa welekeo hali iliyosababisha dereva kulipeleka upande wa kulia ambapo lilipinduka.

Hata hivyo akizungumza baadaye Ofisa Habari na Mawasiliano wa CUF, Silas Bwire alisema hali ya Naibu Katibu huyo ilikuwa ikiendelea vizuri na walikuwa wamepelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu na kuwa walioumia ni watu wawili kati ya watano waliokuwa naye.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo hakuweza kupatikana mara moja kwa maelezo kuwa alikuwa na ugeni katika maadhimisho ya sherehe za Nane Nane.

Sita wauawa Singida
Wakati huohuo  Mwandishi Gaspar Andrew  kutoka Singida anaripoti kwamba watu sita  wameuawa kwa tuhuma za kuteka magari kwenye Mlima Sekenke Barabara Kuu ya Singida kwenda Igunga jana saa 12 jioni.

Ofisa  upelelezi wa mkoa,  Ayub Kenge alithibitisha tukio hilo na kusisitiza kwamba Kamanda wa Polisi Mkoa huo  atatoa taarifa zaidi leo asubuhi.Waliouawa hawakujulikana majina yao, lakini  miili yao ilifikishwa Hospitali ya Mkoa wa Singida na kwamba katika tukio hilo walikutwa na bunduki pamoja na magazine tano zenye risasi 105 pamoja na mabomu saba ya kutupa kwa mikono.

No comments:

Post a Comment