Tuesday, August 9, 2011

Warembo Miss Tanzania waingia kambini




Monday, 08 August 2011 20:47

WAREMBO 30 kutoka kanda tofauti nchini  jana walianza rasmi kambi ya Vodacom Miss Tanzania 2011 kwa ajili ya fainali zilizopangwa kufanyika Septemba 10 kwenye ukumbi wa Mlimani City  jijini.

Mkuu wa Udhamini wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, George Rwehumbiza alisema kuwa sababu kubwa ya kuanzisha utaratibu mpya ni kuwapa nafasi zaidi warembo hao kujifunza mambo mengi wakiwa kambini kama mashindano ya “Big Brother Africa”.

Rwehumbiza alisema kuwa mfumo huu ni tofauti na  ule uliozoeleka miaka ya nyuma ambapo warembo walikuwa wakikaa kambini katika hoteli.

Vodacom Miss Tanzania kwa miaka kadhaa mfululizo safari hii wamebadilisha kabisa muundo wa awali na hivyo walimbwende hao watakaa ndani ya jumba maalum lililopewa jina ‘Vodacom House’ iliyopo maeneo ya Mikocheni jijini.

Alisema kuwa lengo la kufikiwa kwa mabadiliko hayo ni kulifanya shindano hilo liwe na muonekano tofauti kama ilivyo kwa Vodacom ambayo imebadili muonekano wake na kasi ya utoaji huduma.

“Safari hii warembo 30 wanaoshiriki shindano hili la Vodacom Miss Tanzania watawekwa kwenye jumba maalum ‘Vodacom House’ na humo watafundishwa vitu mbalimbali ikiwemo jinsi ya kukabiliana na vishawishi hususan katika masuala ya kimapenzi,” alisema Rweyumbiza.

Akitaja malengo mengine ya kuwaweka washiriki hao ndani ya jumba hilo mkuu huyo wa udhamini alisema kampuni yake kwa sasa inatoa huduma kwa teknolojia yenye kasi zaidi hivyo warembo hawana budi kuendana nayo kwa kufundishwa aina ya kula, kuondoa ulimbukeni mara wanapopata umaarufu.

Mabadiliko haya yatalifanya shindano hili kuwa bora na linaloenda na wakati kama zilivyo huduma zetu yaliyotokana na mabadiliko ya nembo yetu. Wakiwa ndani ya jumba warembo watakaa kwa wiki tatu wakijifunza masuala ya kijamii, alisema Rweyumbiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Lino Agency waandaaji wa shindano hilo Hashim Lundenga amesema kwa mwaka huu wanataka warembo wenye sifa ikiwemo elimu, muonekanao na tabia nzuri ili mashindi atakayepatikana aweze kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa.

Lundenga alisema kuwa mwaka huu watakuwa na mfumo tofaut kwa warembo watakao ingia fainali. Alisema baadala ya 10, mwaka huu kuwa 15 ambapo nafasi tano zitachukuliwa na warembo waliofanya vizuri katika  mashindano maalum ya vipaji, michezo, muonekano katika picha (miss photogenic), Top Model na mrembo mwenye ushirikiano na mchangamfu (Miss Personality).

“Sisi hatuangalii mshiriki ametoka wapi hapa iwe kijijini au mjini, tunachozingatia ni mrembo kukidhi viwango vya shindano ikiwemo sifa tunazozitaka ili mwisho wa siku kila mtu ajivunie mafanikio aliyoyapata akiwa ndani ya jumba la Vodacom House na atumie kigezo hicho kufanikiwa kimaisha,” alisema Lundenga.

Ili kuishirikisha jamii, maisha ya washiriki hao wa Vodacom Miss Tanzania 2011 ndani ya Vodacom House yatakuwa yakioneshwa moja kwa moja ‘Live’ na vituo vya Startv pamoja na Clouds TV ili kutoa nafasi kwa watazamaji kumpigia kura mrembo anayefaa kuvikwa taji hilo na kumrithi Genevieve Mpangala mshindi anayemaliza muda wake.

No comments:

Post a Comment