Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Chadema, Zitto Kabwe na Amos Makala (CCM-Mvomero) ni miongoni mwa wabunge mashuhuri walioteuliwa na Kamati ya Utendaji ya Simba kuunda kamati mbalimbali kuiongoza klabu hiyo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alitangaza kamati hizo jana kuwa lengo hasa ni kusimamia uwekezaji katika klabu hiyo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa klabu pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyoko Mtaa wa Msimbazi.
Mbali na wabunge hao, wabunge wengine waliotajwa kwenye kamati za Simba ni Abdul Mteketa (CCM-Kilosa), Murtaza Ally Mangungu (CCM-Kilwa Kaskazini) na Amos Makala wa CCM-Mvomero.
Rage alisema kamati zilizoundwa ni Fedha, Mashindano, Ufundi, Usajili na Nidhamu ambazo zote kwa ujumla wake zitakuwa na wajumbe 38. Kabwe atakuwa kwenye Kamati ya Fedha itakayoongozwa na Geofrey Nyange 'Kaburu', Adam Mgoi (Makamu), Said Pamba, Juma Pinto, Mtekete, Mangungu na Kifiri.
Makala atakuwa kwenye Kamati ya Mashindano itakayoongozwa na Joseph Itang'are (Mwenyekiti), Azim Dewji (Makamu), Jerry Amri, Swedy Mkwabi, Hassan Hasanoo, Mohamed Nasor, Richard Ndassa na Suleiman Zakazaka. Awali ilikuwa chini ya Danny Manembe.
Kamati ya Ufundi itaongozwa na Ibrahim Masoud, Evans Aveva (Makamu), Dan Manembe, Khalid Abeid, Musley Ruwey, Mulamu Ng'ambi, Said Tuli, Rodney Chiduo na Patrick Rweyemamu.
Rage aliitaja Kamati ya Usajili itakayokuwa chini ya mwenyekiti wake, Hans Pope, Kassim Dewji (Makamu), Fransis Waya, Crescentius Magori, Salim Abdallah, Collins Frisch na Gerald Lukumay.
Mwenyekiti huyo wa Simba ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini-CCM, alisema Kamati ya Nidhamu itaundwa na Peter Swai (Mwenyekiti), Jamal Rwambow (Makamu), Charles Kenyela, Evod Mmanda na Chaurembo Abdalah.
Rage alisema uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo umezingatia vigezo na uwezo waliona katika upeo mpana wa kuiendeleza Simba, na masuala makuu mawili ni Uwekezaji na Uwanja ndio msingi wa kuundwa kwake.
Mwenyekiti huyo alisema anaamini wajumbe na kamati watakazosimamia watakafanya kazi kwa ushirikiano ili kutekeleza na maazimio yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba umesema utalibomoa jengo la klabu hiyo kupisha ujenzi wa ghorofa 10 za kisasa katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Msimbazi na Aggrey.
Rage alisema jana kuwa klabu yake imedhamiria kutumia nguvu nyingi katika uwekezaji ili kuendana na wakati. "Tuko katika mazungumzo na benki mbili, na mazungumzo yanakwenda vizuri, na yakikamilika, ujenzi utaanza mapema mwakani."
Kuhusu ujenzi wa uwanja uliopo Bunju, nje kidogo ya jiji, alisema mipango inaendelea vizuri.
Aidha akizungumzia suala la nembo ya klabu hiyo, alisema bado wanaendelea na taratibu za kuhakikisha vifaa vyenye nembo yao vinauzwa kihalali. |
No comments:
Post a Comment