Na Mwandishi Wetu,jijini
KOCHA Mkuu wa Simba Mganda Moses Basena amesema kwamba mechi moja tu ya kirafiki katika timu yake, itamsaidia kupata kikosi cha kwanza katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, inayotarajiwa kuchezwa Mei 28 mwaka huu,jijini Cairo.
Timu ya Simba imeondoka jijini leo kwenda visiwani Zanzibar kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo, kabla ya kuondoka Jumatano ijayo kwenda nchini Misri.
"Tukiwa Zanzibar nitatafuta japo mechi moja ya majaribio ili niweze kuangalia kikosi changu, kwasababu ndiyo kwanza naanza kukinoa ila sitafanya mabadiliko makubwa sana na kile cha zamani," amesema Basena.
Amesema kambi wanayokwenda kuweka Zanzibar itamsaidia sana kukaa na wachezaji wake pamoja, kwani itamsaidia kujua uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Basena amesema kwa jinsi alivyowaona wachezaji wake mazoezini, amegundua kwamba wachezaji wanauwezo mkubwa na kinachotakiwa ni kuwapa mazoezi zaidi ili wawe fiti muda wote.
Karibu wachezaji wote wa Simba wamesharipoti mazoezini, isipokuwa Mbwana Samatta ambaye yupo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na timu yake a TP Mazembe, na uongozi wa Simba bado unaendelea kuiomba timu hiyo ili wamwachie mchezaji huyo aungane na wenzake katika michuano hiyo ya klabu bingwa. |
No comments:
Post a Comment