Na Masau Bwire,jijini
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Kigogo iliyopo Manispaa ya Kinondoni wamepanga kuandamana kwenda Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kupinga kuwepo kwa nyumba ya kulala wageni bubu, ndani ya eneo la shule yao.
Wamedai kuwepo kwa gesti hiyo ni kikwazo kikubwa katika masomo yao na ustawi wa maadili mema kwa watoto.
Wakizungumza na Dar leo shuleni hapo jana, wanafunzi hao walisema, mbali na kuzitaarifu mamlaka husika kuhusu athari za kuwepo kwa gesti hiyo bubu ndani ya shule yao na azma yao ya kutaka iondolewe katika eneo la shule yao.
Mamlaka hizo zimekuwa kimya na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, hali ambayo walisema, imewasukuma kufanya maandamano ya amani kwenda kwa Rais Kikwete kumweleza kero hiyo ili awasaidie, kwa kuwa, watendaji wa chini yake, wameshindwa kuwasaidia.
Wakizungumza kwa jazba wanafunzi hao walisema, makelele ya kila siku ya wateja wa gesti hiyo wakati wa masomo, ambao hukurupushana kutoka vyumbani wengine wakiwa wamevaa tu nguo za ndani, yanawaathiri sana kimasomo na kimaadili kwani, hupoteza kabisa usikivu darasani na umakini wa kujifunza.
"Asubuhi tukiwa shuleni tukiimba wimbo wa Taifa, ghafla mbele yetu hutokea wateja wa gesti hiyo, mke na mume tena wakati mwingine wakiwa wamevalia nguo za ndani tu, wakigombana kwa sauti kubwa na matusi ya nguoni, hali ambayo inatuweka katika wakati mgumu kitaaluma na kimaadili," amesema Yasin Abasi wa kidato cha pili.
Walisema, miongoni mwa wateja wa gesti hiyo ambao huwashuhudia wakiingia na kutoka ndani ya gesti hiyo ni watoto wadogo wa kike wa rika lao, ambao huwa na mafataki inayowaingiza humo ili kujistarehesha kwa ngono.
"Hali ya kushuhudia wasichana wadogo wa rika letu wakiingia na kutoka ndani ya gesti hiyo na wanaume wenye umri mkubwa sawa na baba zao, kwetu ni aibu na fedheha na pia inaweza kuwa kishawishi kwa wanafunzi wengine wenye tamaa ya mali na mtazamo hasi kwa kujiingiza katika vitendo hivyo vya kikahaba," amesema mwanafunzi mmoja, Johari Maulidi wa kidato cha tatu.
Walisema wakati mwingine hushuhudia yanayofanyika ndani ya vyumba vya gesti hiyo, kwani madirisha yake yako wazi, hayana pazia wala kizuizi chochote cha kufanya yaliyomo ndani yasionekana kwa watu wa nje.
Wanafunzi hao walisema, pamoja na athari za kitaaluma na kimaadili, pia, wanaathirika kiafya kwani, wanapofanya usafi wa eneo la shule yao, hulazimika kuokota mipira ya kiume iliyotumika.
Wanafunzi hao walisema, kabla ya kufanya maandamano hayo siku chache zijazo, watafanya hamasa kwa wazazi wao, wadau wa elimu na asasi za kijamii zinazojishughulisha na masuala ya elimu na haki za mtoto ili wawaunge mkono katika maandamano yao.
Wanafunzi hao walihoji kwamba, inakuwaje Waziri wa Ujenzi, John Magufuli anaweza kuvunja maghorofa yaliyojengwa ndani ya hifadhi ya barabara zake, wakati wengine wanashindwa kuvunja nyumba tu ya kawaida ambayo imejengwa ndani ya eneo la shule.
Diwani wa kata hiyo, Richard Chengula, amekiri kuwepo kwa gesti hiyo bubu ndani ya eneo la shule hiyo na kudai, Serikali ya mtaa husika imesimamisha huduma za gesti hiyo kuanzia juzi.
Mbali na serikali ya mtaa kusimamisha huduma, lakini Dar Leo lilishuhudia wateja kadhaa wakiingia na kutoka ndani ya gesti hiyo.
Mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo, ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliyedai ameajiriwa kwa kazi ya usafi ndani ya gesti hiyo, alisema gesti hiyo ipo kwa mujibu wa sheria, imesajiliwa na Serikali ya Tanzania kwa jina la The Queen Guest House na kwamba, leseni yake ya biashara imelipiwa haina matatizo ya aina yoyote. |
No comments:
Post a Comment