Sunday, May 22, 2011

YANGA WAUNGANA NA SIMBA KLABU BINGWA AFRIKA

Friday, 20 May 2011 09:25
Na Elizabeth Mayemba,jijini

UONGOZI wa klabu ya Yanga umewatakia kila lakheri watani zao Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kushinda rufaa yao dhidi ya TP Mazembe ya congo, baada ya kumchezesha mchezaji batili na kuwataka waitumie vizuri nafasi hiyo.

Mei 28 mwaka huu, timu ya Simba inatarajiwa kucheza mchezo wake wa
klabu bingwa dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, katika Uwanja wa PetroSport jijini Cairo.

Akizungumza na Dar Leo, leo asubuhi Msemaji wa klabu ya Yanga Louis Sendeu amesema, pamoja na upinzani mkubwa walionao wa wenzao wa Simba, katika michuno hii wanaungananao na wanaiombea ifike mbali katika michuano hiyo.

'Sisi tupo nyuma yao na tunawatakiwa kila lakheri wafanye vizuri katika michuano hiyo ili wafike mbali, kwa kuwa bahati imewaangukia hivyo wasiichezee," amesema Sendeu.

Amesema kwa hili wanaweka uzalendo mbele na kuungana nao kipindi chote watakachokuwa katika mashindano hayo.

Katika mchezo huo iwapo dakika 90 zitamalizika kwa sare, mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penalti, na iwapo Simba watashinda watakuwa kundi B na timu za Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia na MC Alger ya Algeria.

Lakini kama Simba watashindwa katika mechi hiyo itacheza raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho (CAF), na wakishinda wataingia katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment