Thursday, July 14, 2011

Baada ya Rostam Aziz kujivua gamba, Wabunge Chadema, CCM wachekelea

 
Wednesday, 13 July 2011 20:53

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe
Leon Bahati, Dodoma na Moses Mashalla, Arusha
WABUNGE na CCM na Chadema wameonekana kufurahia kujiuzulu kwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Kufuatia hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, alisema: “Sisi tumefurahi kwamba kuna jimbo lipo wazi na tutalichukua kwenye uchaguzi mdogo”.

Hata hivyo, kupitia ujumbe wake wa simu ya mkononi, Zitto alisema asingependa kuzungumzia suala hilo zaidi kwasababu haliwahusu Chadema bali ni la CCM.

Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema bado gamba la CCM halijavuka kwa sababu Rostam ni mmoja wa watuhumiwa 11 waliotajwa na Chadema kwenye orodha ya watuhumiwa wa ufisadi, Mwembeyanga mwaka 2007."Bado kumi," alisema Lissu huku akijigamba kuwa mafanikio hayo ni juhudi zilizofanywa na Chadema ili kulinda raslimali za Watanzania.

Kuhusu kauli ya Rostam kuwa amejing'oa kwenye nyadhifa zake kutokana na siasa uchwara, Lissu alisema: "Kama kweli siasa uchwara ndizo zimemwondoa Rostam, basi ndizo zinazolifaa kuendelezwa hapa nchini."

Nwa Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei, alisema kujivua gamba kwa Rostam hakuwezi  kuiokoa CCM kujinasua katika tope la ufisadi na kwamba, kujiondoa kwake ni kama tone la maji ndani ya Bahari la Hindi.

Mtei alisema kuwa kujiondoa kwa Rostam ni dalili za kuangamia kwa chama hicho tawala na kusisitiza kwamba, CCM si chama cha kujisafisha bali ni chama kinachojifia taratibu bila kujijua. Aliongeza kuwa ufisadi uko kwa watakaoachwa na Rostam.

Wabunge wa CCM
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole-Sendeka, alisema kujivua kofia zote alizokuwa nazo ni kitendo cha kukiletea afya chama hicho tawala.Alisema kuwepo kwa vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa ndani ya CCM, ili chama kipone lazima waondoke.

Alisema anamuunga mkono Rostam kwa uamuzi aliuchukua wa kutii mkakati wa chama wa kujivua gamba na kwamba, hiyo ni hatua moja ya kukiboresha chama."Unaposhauriwa kwa afya ya chama chako na ukakubali ni uamuzi wa kijasiri," alisema Ole-Sendeka. Lakini alionya kuwa mkakati huo wa kujivua gamba ni zaidi ya vigogo watatu ambao wamekuwa wakitajwa mara kwa mara.

Alisema wote wakifuata mkondo wa Rostam, kutakijengea chama taswira nzuri ya kupendwa na watu ambao tayari wameanza kukata tamaa kutokana tuhuma zinazowahusu.

Alipoulizwa ana wito gani kuhusu wale ambao bado hawajatekeleza hilo, Ole-Sendeka alisema: "Cheo ni dhamana, uongozi ni utumishi, kama waliokupa dhamana wanakushauri uondoke, huna haja ya kubishana nao, tekeleza."Naye Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini-CCM), alisema amefurahishwa na hatua ya Rostam kuachia ngazi kwa lengo la kusafisha chama.

"Sasa ni wakati kwa wengine kuchukua uamuzi kama huo. Tunajua wako wengi, waondoke ili chama kiimarike," alisema Mohamed.
venance.chadema@yahoo.com

No comments:

Post a Comment