venance.chadema@yahoo.com
Friday, 12 August 2011 21:43 |
Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu Waandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imesitisha leseni ya biashara ya Kampuni ya Mafuta ya BP kwa miezi mitatu kwa kukaidi agizo lake la kutoa huduma ya uuzaji wa mafuta.Imesema Bodi yake ya Wakurugenzi imeagiza Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa kampuni hiyo pekee ya mafuta ambayo Serikali ina hisa asilimia 49, afikishwe mahakamani kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP) kwa kukaidi agizo hilo la Ewura.
Pia, imezipa onyo kali Kampuni za Oilcom, Camel Oil na Engen na kuzitaka kutorudia tabia ya kugoma kupunguza bei ya mafuta kwa kuwa ni kinyume na sheria za Tanzania, huku ikiwataka kuuza mafuta kama awali kwa watu wote bila ubaguzi.Rungu hilo la Ewura linakuja takriban wiki moja baada ya wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza nishati hiyo kwa bei elekezi ya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu alisema uamuzi wa kuifungia BP umetolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo jana mchana.
“Uamuzi tuliochukua ni kusitisha leseni ya biashara ya BP kuuza kwa jumla mafuta ya dizeli, petroli na taa kwa miezi mitatu kuanzia leo (jana),” alisema Masebu.
Alisisitiza kwamba Ewura itafuatilia kwa makini utekelezaji wa amri hiyo na ikibainika wanaendelea kukiuka, watachukuliwa hatua kali zaidi.
Hata hivyo, Masebu alisema kampuni ya BP itaruhusiwa kuendelea kuuza mafuta ya ndege kutokana na ukweli kwamba Ewura haidhibiti bei za mafuta hayo.
“Hii inafanyika ili kuzuia kutoharibika kwa mafuta hayo katika kipindi hicho cha miezi mitatu ambacho hawataruhusiwa kufanya biashara ya mafuta ya jumla.”
Alisema kuwa vituo vyote vya rejareja vyenye nembo ya BP vitaruhusiwa kuuza mafuta kwa kununua kwa wafanyabiashara wengine wa jumla.“Bodi imeagiza Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa BP kufikishwa mahakamani kwa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP),” alisema Masebu.
Alisema Ewura itaendelea kusimamia mfumo mzima wa mafuta yanayoingia bandarini pamoja na kufuatilia bei zinazouzwa kwenye vituo kama zinafanana na zile zilizotangazwa.
FCC yaendelea kuzibana
Kampuni zote za mafuta zilizoadhibiwa na na Ewura zipo hatarini kuadhibiwa mara mbili baada ya Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC), kusema kwamba inaendelea kuchunguza iwapo zimevunja Sheria ya Ushindani wa Biashara.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mkurugenzi wa Sheria wa FCC, Gregory Ndanu aliliambia gazeti hili kuwa wameanza uchunguzi kwa kampuni hizo na ile itakayotiwa hatiani itakabiliwa na faini ya mamilioni ya fedha kulingana na wastani wa mapato yake kwa mwaka.
Uchunguzi huo unatokana na mgomo wa kampuni hizo kutoa huduma nchini kwa karibu siku 10, zikiilazimisha Serikali isipunguze bei ya dizeli, petroli na mafuta ya taa.“Uchunguzi bado tunaendelea nao kama kawaida ila uamuzi wa mwisho utatolewa na bodi (ya FCC),” alisema Ndanu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na FCC wiki hii ilieleza kuwa tume hiyo ina wajibu wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanafaidika na mfumo wa biashara huria nchini.
Kwa sababu hiyo, pale FCC itakapobaini kuwa wafanyabiashara wanavunja Sheria ya Biashara ya Ushindani kwa kugoma kwa pamoja, kutoa masharti ya pamoja au kupanga bei ya soko, watachukuliwa hatua.
Kabla ya taarifa hiyo, Ndanu alikuwa amesema kuwa kampuni inayopatikana na hatia ya kuvunja sheria hiyo, hutozwa faini ya asilimia tano hadi 10 ya mapato yake yote kwa mwaka uliotangulia.
Alisema kampuni yoyote inayokiuka ushindani wa biashara inaadhibiwa kwa mujibu wa Sheria namba 9 ya mwaka 2003 kifungu cha 1(a), (b), (c) na (d) ambayo inakataza aina yoyote ya wafanyabiashara kushirikiana ili kulazimisha mwelekeo wa bei sokoni.
Kampuni zilivyogoma
Baada ya Ewura kutangaza bei mpya ya mafuta iliyoanza Agosti 3, mwaka huu, kampuni zilianza mgomo baridi wa kutouza mafuta kutoka kwenye maghala yake.
Sakata hilo liliifanya Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura kukutana Agosti 9, mwaka huu na kutoa agizo la kisheria kwa kampuni nne ambazo zilionekana kinara wa mgomo huo ambazo ni BP, Oilcom, Camel na Engen.Baada ya agizo hilo kampuni tatu kati ya hizo zilitii amri isipokuwa BP ambayo imegoma kuuza mafuta mpaka sasa.
Tangu kuanza kwa mgomo wa uuzaji wa mafuta vituo mbalimbali vya BP Dar es Salaam, vilisitisha kutoa huduma ya uuzaji wa mafuta.
|
No comments:
Post a Comment