Tuesday, August 9, 2011

Fundisho: Rooney ajipanga kuitesa zaidi Man City.

Imewekwa:: 2011-08-09 09:38:00



Nyota wa Manchester United, Wayne Rooney
LONDON, ENGLAND
NYOTA wa Manchester United, Wayne Rooney amesema kikosi chake kimetoa somo kubwa kwa majirani zao baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwenye mechi ya kuwania Ngao ya Hisani iliyochezwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Wembley.

Manchester City walikuwa mbele kwa mabao 2-0 lakini Manchester United walikaza msuli na kufunga mabao matatu.

"Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani timu yetu ni bora,''alisema Rooney "Tulitawala mechi nzima, tumewaonyesha kwamba sisi ni zaidi. Sisi ni mabingwa na tulitaka kuthibitisha hilo.

Rooney aliongeza; "Ushindi huu ni mtamu kwa sababu tumelipa kisasi baada ya kufungwa katika nusu fainali ya Kombe la FA katika Uwanja wa Wembley msimu uliopita."

Naye kocha wa Manchester United, Alex Ferguson, alisema kitu kilichomfurahisha ni kuona vijana chipukizi wakifanya mashambulizi ya maana.

Katika kipindi cha pili aliingiza wachezaji watatu Phil Jones, Jonny Evans na Tom Cleverley, ambao walionyesha kiwango kizuri na alipomtoa Patrice Evra na kumwingiza Rafael da Silva dakika ya 71 wastani wa miaka katika kikosi ulikuwa 22.

"Watu walikuwa wakisema timu yetu ya sasa si nzuri, nadhani tumethibitisha ubora. Nataka niwakumbushe watu kuwa wachezaji chipukizi watatisha msimu huu.

Naye kocha wa Manchester City, Roberto Mancini, amesema timu yake inatakiwa kukuza ari.

"Ni kweli majirani zetu walicheza zaidi yetu. Kwa kawaida unapokuwa juu kwa mabao 2-0 unatakiwa kulinda mabao na kutafuta mengine kwa juhudi."

No comments:

Post a Comment