Tuesday, August 9, 2011

SIMBA DAY: Simba! Simba! Aaah!

venance.chadema@yahoo.com


Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange akichezea timu ya viongozi wa Simba, akimdhibiti Abdallah Ally wa timu ya makocha wa Arusha, Imam Ally wakati wa mechi ya ufunguzi wa Simba Day kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana Jumatatu.
MICHAEL MOMBURI,ARUSHA
SIMBA..Simba! Aaah! Ndiyo kilichotokea wakati mashabiki wa Simba wakishangilia pasi za timu yao ilipocheza na Victors ya Uganda lakini ghafla wakanywea.

Kikosi kikicheza kwa mara ya kwanza kikiwa kamili baada ya usajili kukamilika ndani ya ardhi ya Tanzania Bara, Simba ilionyesha mabadiliko lakini ikalala kwa bao 1-0 mbele ya Victors ya Uganda jana Jumatatu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kocha Moses Basena alilaumu washambuliaji wake kwa kuwataja kwa majina Uhuru Seleman, Emanuel Okwi na Felix Sunzu kwa kukosa nafasi za wazi ambazo zingeweza kuwapa raha zaidi mashabiki katika mchezo huo ambao beki wa zamani wa Simba, Joseph Owino alikuwa jukwaani akishuhudia.

�Kwa nafasi kama alizopata Uhuru, Sunzu yalikuwa ni magoli ya wazi walihitaji utulivu, lakini timu imeonyesha mabadiliko ingawa tumepoteza tunahitaji kubadilika na kujipanga zaidi kwa kuongeza umakini,�alisema Basena.

�Ukiangalia katika ulinzi bado hakuna uelewano mzuri kati ya Mungusa na Costa lakini ni sehemu ambazo tunahitaji kuzifanyia kazi na watu waelewe kwamba kuna wachezaji wako nje katika kambi ya Taifa Stars na wengine ni majeruhi, wasikate tamaa,�alisisitiza.

Mechi hiyo ya Simba Day ilikuwa ni ya kwanza kikosi cha Simba kuonekana Bara baada ya kutangaza usajili ambapo, katika kambi yake ya Zanzibar ilicheza mechi mbili dhidi ya Polisi na Karume Boys na kushinda zote.

Simba ilionyesha kiwango kikubwa na soka la burudani kwa kushambulia vizuri na kufanya mambo ya aina yake ingawa bado mastraika wake wanne walishindwa kufumania nyavu dakika 45 za kwanza.

Kitendo cha beki mpya wa Simba, Victor Costa kumkwatua Abdallah Mohamed dakika ya 57 kilisababisha penalti ambayo Sebuguzi Eric alimfunga Juma Kaseja kiulaini dakika ya 59.

Katika kikosi cha jana ambacho mbele kilikuwa na Mzambia Felix Sunzu, Mganda Emanuel Okwi, Gervais Kago wa Afrika ya Kati na Haruna Moshi waliotengeneza nafasi zaidi ya tano lakini umaliziaji ulikuwa tatizo ingawa mabeki wa Victors walifanya kazi kubwa pia.

Kago, ambaye katika mechi mbili zilizopita alipachika mabao, alikosa nafasi nyingi za wazi alizotengewa na Sunzu na kufanya Basena kumtoa kipindi cha pili na kumuingiza Uhuru Suleiman ambaye alionyesha kwamba amepona majeraha.

Victors walikuwa na ukuta mzito chini ya kipa Kimera Ally, ambapo wachezaji wengi wa timu hiyo walicheza pasi fupi kwa kasi huku winga zote zikionyesha uhai jambo ambalo lilisababisha wakati mgumu kwa mabeki Costa na Obadia Mungusa.

Hata hivyo, Mungusa alitolewa kipindi cha pili akaingia Kelvin Yondani. Sunzu ambaye alipachika bao dakika ya 44 kwa shuti kali lakini mwamuzi Judith Gamba wa Dar es Salaam alilikataa kwa maelezo kuwa aliotea.

Hiyo ni mechi ya tatu kwa Sunzu kuichezea Simba bila kufunga bao ingawa zote ni za kirafiki dhidi ya Polisi, Karume na Victors lakini amewaambia mashabiki wasiwe na wasiwasi yuko fiti na anahitaji muda jambo ambalo hata kocha Basena aliliunga mkono.

Basena alisema wachezaji hao wamecheza vizuri huku akisisitiza kuwa yalikuwa ni majaribio mazuri kwake wala hana wasiwasi.

Simba inajiandaa na mechi dhidi ya Yanga Agosti 17 kwenye Ngao ya Hisani pamoja na ile ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro mjini hapa Agosti 21.

Kikosi cha Simba kilikuwa hivi: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Nasoro Cholo,Obadia Mungusa/Kelvin Yondani, Victor Costa, Patrick Mafisango/Abdala Sesema, Gervas Kago/Uhuru Seleman, Shomari Kapombe,Felix Sunzu/Rashid Ismail,Haruna Moshi,Emmanuel Okwi.

No comments:

Post a Comment