Waandishi wetu, Dodoma, Dar
LICHA ya kupata wakati mgumu Bungeni, Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imepitishwa jana huku Waziri wake, Profesa Anna Tibaijuka akitoa onyo kwa wanaohodhi ardhi kwa muda mrefu bila kuiendeleza akisema: “Fungate yao imekwisha.”
Kauli hiyo ya Profesa Tibaijuka imekuja siku moja baada ya kambi ya upinzani bungeni kupitia Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee kutaja orodha ndefu ya vigogo hao wa CCM wakiwamo Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Mawaziri Wakuu wastaafu, John Malecela na Frederick Sumaye.
Wengine waliotajwa ni Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula na aliyekuwa Naibu wake (Bara), Hassan Ngwilizi akisema kwamba wamehodhi ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuiendeleza. Hata hivyo, alisema ni
Mkapa pekee aliyeendeleza eneo lake.
Mwingine aliyetajwa na Mdee ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Nawab Mulla.Akijibu hoja hiyo na nyingine bungeni jana Profesa Tibaijuka, kwa kifupi alisema kwa wamiliki wote wa ardhi ambayo haijaendelezwa: “Honeymoon is over” (fungate imekwisha) na kwamba wizara yake itapitia miliki za mashamba na maeneo mengine yasiyoendelezwa kisha kuchukua hatua stahili.
“Wizara yangu itafanyia ukaguzi maeneo haya ya ardhi, hivyo wanaomiliki mashamba ambayo bado hayajaendelezwa basi wajue kwamba “honeymoon is over."
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema) katika hoja hiyo, alisema vigogo hao wanahodhi maeneo makubwa ya ardhi huku wananchi hasa wale waishio jirani nayo wakikosa ardhi hali ambayo aliita ni hatari kwa amani ya nchi.
Bila kuwataja kwa majina vigogo hao kwa majina kama alivyofanya waziri kivuli, Profesa Tibaijuka pia alisema kwamba hata wale ambao wamemilikishwa ardhi na kuamua kuikodisha kwa wananchi na kuwatoza kodi, watashughulikiwa.
Pinda aingilia kati
Kabla ya Waziri Tibaijuka kujibu hoja za wabunge, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alizungumza na kueleza kuwa mgogoro wa ardhi ambao umekuwa ukipigiwa kelele na Watanzania kuhusu shamba la Katumba, anaufahamu na kwamba upo kwa maslahi ya wananchi wa maeneo hayo.
Alisema Shamba la Katumba halina mgogoro, bali wanaopiga kelele ni watu wanaotoka mbali na maeneo kwani hawajui msingi wa mkataba huo.
“Waheshimiwa wabunge, eneo la Katumba liko jimboni mwangu na mara nyingi watu wanapopiga kelele hapa siwaelewi na siko tayari kukubaliana nao, nitaufia msimamo wangu kuhusu eneo lile,’’ alisema na kuongeza:
“Kama kuna kitu ambacho lazima wenzetu wakubali ni pamoja na kuwa mikoa ya pembezoni ilikuwa nyumba sana licha ya kuwa sisi ndiyo tunaolisha Tanzania nzima. Sasa hatukubali.”
Alisema bado mwekezaji hajapewa idhini ya kumiliki kama ambavyo wengi wamekuwa wakieneza na badala akasema ni makubaliano ya awali tu ndiyo yaliyofanyika ambayo yatakwenda hatua nyingine tena kwa kushirikisha vyombo husika.
Alieleza kusikitishwa kwake na jinsi baadhi ya watu wanavyojia juu hatua hiyo ya kuwekeza katika shamba hilo na maeneo ya pembezoni jambo ambalo pia linafanyika katika maeneo mengine ya nchi.Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, Pinda alikiri kuwa ipo kutokana na wananchi wengi kuhitaji ardhi na akasema jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa umakini.
Hata hivyo, licha ya kumsifia Profesa Tibaijuka, aliwataka mawaziri pia kuwa na meno kwa watendaji wao kuliko kuendelea kulalamika kila siku.
“Nataka kuwaambia mawaziri wote kuwa acheni kunung’unika juu ya watendaji wabovu, nendeni mkafoke ikibidi watimueni halafu mambo mengine yatafuata ili mradi mfuate taratibu na sheria za kutomuonea mtu,’’ alisema.
Michango ya wabunge
Wabunge wengi waliochangia mjadala wa hotuba hiyo walituhumu baadhi ya mambo ikiwamo rushwa katika sekta ya ardhi nchini na kuonyesha kuchukizwa kwao na ufisadi unaotikisa sekta hiyo kwa kuhusisha maofisa ardhi, kuchelewa kesi mahakamani zinazohusu migogoro ya ardhi na bajeti finyu ambayo ya Sh47.89 bilioni ambayo walisema haiwezi kuleta tija katika mabaraza ya ardhi.
Mdee aonya machafuko kugombea ardhi
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliitahadharisha Serikali kuwa kuipuuza sekta ya ardhi kutasababisha watu wa taifa hili kuchinjana.“Sekta ya ardhi ndiyo uhai wa nchi hii. Sekta hii tukiipuuza... na ninaiambia Serikali tukiipuuza watoto wetu, wajukuu wetu watakuja kuchinjana na hatutaki kutengeneza Tanzania ya kuchinjana katika kipindi,” alisema Mdee.
Akizungumzia kuhusiana na Kampuni ya Agri Soil ambayo imepewa eneo la uwekezaji katika Wilaya ya Mpanda, Mdee alisema mbali na upungufu wake imekiuka sheria.“Imekiuka sheria ya nchi, sheria zetu zote ziko wazi na hili namwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu asiposhughulikia vizuri anaweza akaanguka nalo kabisa kwa sababu kuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa ofisi yake ilihusika tutumie busara tuokoe nchi,” alisema.
Mdee alisema sheria inasema kama kuna ushirikiano unamhusu raia na kwamba sheria ya uraia haijatambua halmashauri na kuhoji kuwa Serikali iwaambie wabunge ni raia gani anamiliki hekta zaidi ya 200?
Mgogoro wa shamba hilo uliibukia kwa mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Pudenciana Kikwembe ambaye aliitaka serikali kutoa asilimia 25 ya hisa katika shamba hilo kwa wazawa na kwa sababu madiwani walishirikishwa katika suala la Agro Soil basi waamue gawio la faida litakwenda katika mradi gani.
Mbunge wa Nkenge (CCM), Assumpta Mshama alilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwachukulia hatua watu waliojilimbikizia ardhi pasipo kufanyia shughuli za maendeleo.
“Naiomba wizara ichukue maoni kwa wananchi kujua ni kwa namna gani wanafaidika na hao wanaojiita wawekezaji waliopewa sehemu kubwa ya ardhi kuliko kuwaachia watu wasiowanufaisha wananchi husika.”
Mshama aliwataka mahakimu wasiendeshe kesi za migogoro ya ardhi kwa muda mrefu ili kuwapatia hati stahiki walalamikaji kwa muda muafaka kwa ajili ya kujiletea maendeleo kiuchumi.
Mbunge wa Babati Vijijini (CCM), Jitu Soni alisema jimbo lake limekumbwa na mgogoro wa Bonde la Mto Kilwa kwa zaidi ya miaka 25 bila usuluhishi wowote.“Tume mbalimbali zimekuwa zikiundwa kujadili tatizo hili, lakini kwa kipindi chote hicho zinakuja na majibu yasiyo na muafaka wa tatizo,” alisema.
Mbunge huyo alitoa pendekezo kwamba, ili kupunguza matabaka na umaskini uliokithiri kwa wananchi wengi ni vizuri kila mwananchi anayemiliki ardhi apimiwe eneo lake na apewe hati miliki.“Endapo suluhisho la matatizo haya ya ardhi litafanikiwa, utabaka utatoweka na hali ya umaskini itapungua. Watu wanahitaji ardhi kwa ajili ya kujijenga kiuchumi ili waishi vizuri kwa amani hivyo basi, ni vizuri kama kutakuwa na ardhi maalumu zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na makazi.”
Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Philipo alisema asilimia 90 ya kero za wananchi wa jimboni kwake ni migogoro ya ardhi ambayo imesababishwa na wawekezaji wakubwa ambao mikataba yao ilishakwisha malizika siku nyingi bila kufanyiwa ufuatiliaji.
“Naomba wizara ishughulikie mikataba iliyoweka na wawekezaji wakubwa ambayo mingi imeonekana kuisha siku zake, lakini maeneo hayarudishwi kwa wananchi kwa ajili ya kuwanufaisha badala yake wamekuwa wakinyanyasika.”
Alipendekeza kwamba halmashauri ziwezeshwe kwa kupewa vifaa vya upimaji jambo ambalo litawasaidia wananchi kutumia ardhi zao kuchukua mikopo itakayowasaidia kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere kutokana na ufinyu wa bajeti katika wizara hiyo, alimtaka waziri Tibaijuka ajiuzulu wadhifa wake kwa kumwambia Rais ameshindwa kufanya kazi.
“Siungi mkono hoja na naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi uende kwa Rais kumwambia umeshindwa kazi kutokana na fungu kuwa dogo, kama huwezi mimi nitakusaidia,” alisema.
Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse aliitaka Serikali ijilize migogoro ya ardhi inasababishwa na nini? Kwa mtazamo wake, tatizo hilo linatokana na mfumo mbovu uwekezaji na mamlaka iliyopewa dhamana haitendi kazi ipasavyo.
Alizitaka Wizara za Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Kilimo, Chakula na Ushirika na Maliasili na Utalii kukutana kwa ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ardhi kwa wakulima, wafugaji na wananchi wa kawaida.
Mbunge wa Ilemela kwa tiketi ya Chadema, Ezekia Wenje aliwashutumu Mkurugenzi wa jiji la Mwanza kwa kujimilikisha eneo kubwa la ardhi maeneo ya Luchelele kutoka kwa wananchi wa hali ya chini bila kuwapa fidia stahili.
Naye Susan Kiwanga (Viti maalumu, Chadema), alimshutumu Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina akisema amejimilikisha eneo la ardhi linalofikia hekari 300 huko Morogoro huku akijisifia kuwa amewalipa kiasi kidogo cha fedha.
“Inasikitisha sana kuona watu tuliopewa dhamana kutetea haki za wananchi ndiyo tunaongoza kwa kuwanyanyasa. Kwa mfano, Mbunge wa Kisesa ameamua kuja kujimilikisha hekari 300 kutoka kwa wananchi wa hali ya chini huku akijisifia. Ina maana ardhi huko Mwanza imekwisha?’’
Mbali na hilo, Kiwanga alisema migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na rushwa iliyotawala miongoni mwa watendaji lakini pia huku akielezea kushangazwa kwake na kauli ya wizara kwamba ni asilimia moja tu ya ardhi nchi nzima iliyopimwa.
|
No comments:
Post a Comment