Wednesday, August 17, 2011

Chadema waivaa rasmi CCM uchaguzi Igunga

venance.chadema@yahoo.com


Tuesday, 16 August 2011 21:09


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza rasmi mapambano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga baada ya kumwandikia barua msimamizi wa uchaguzi huo kikimtuhumu Mweka Hazina wa chama hicho tawala ngazi ya taifa, Mwigulu Nchemba kuanza kumwaga misaada yenye lengo la kile ilichodai ni kushawishi wapigakura.

Hatua hiyo ya Chadema kuandika barua rasmi kuelezea tuhuma hizo, imekuja wakati tayari vyama hivyo viwili vikiwa katika malumbano ya maneno kila kimoja kikikishutumu kingine kucheza mchezo mchafu kabla ya muda wa kampeni uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Chadema kiliandika barua hiyo yenye kumbukumbu namba  CDM/W/IG/UCH/Vol.1/201 Agosti 15, mwaka huu na kusainiwa na katibu wa chama hicho
Wilaya ya Igunga, Christopher Saye.

Barua hiyo ambayo nakala yake pia imepelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na polisi Wilaya ya Igunga, Chadema kinamtuhumu Mhazini na Mratibu wa huyo Kampeni wa CCM kwenye uchaguzi huo, kwa kutoa fedha kwa vijana wapanda baiskeli ili wapeperushe bendera za chama hicho tawala.

Chadema katika sehemu ya barua hiyo, pia kinadai kuwa Nchemba, mnamo Jumapili ya Agosti 14, alihudhuria misa kwenye Kanisa la KKKT Mjini Igunga ambako alitoa msaada wa Sh2 milioni kwa kwaya ya kanisa hiyo inayoitwa Imani.

Katika barua hiyo, pia Chadema kinamtuhumu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nsimbo, waliyemtaja kwa jina la Rahel Manase na kusema hakina imani naye kikidai kuwa amepita kwa baadhi ya viongozi na wanachama wake na kuwatishia kwamba wasipokihama chama hicho cha upinzani (Chadema), atawashughulikia.

Sehemu ya barua hiyo pia inatoa malalamiko kwa kitendo cha Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Iddy Amme kutokana na kile walichodai ni kwenda katika Kijiji cha Nyandekwa ambako Agosti 13, alipita kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji na kuwanunulia wananchi huku akiwataka kuchagua CCM uchaguzi ukifika.

Chama hicho pia kinadai kuwa wanachama na baadhi ya viongozi wake wameanza kutishwa na kubambikiwa kesi na kutoa mfano kwa mweka hazina wake wa Tawi la Ipumbulya, kukamatwa na kuwekwa ndani siku mbili tangu alipotundika bendera ya chama hicho nyumbani kwake.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimemtaka msimamizi huyo kushughulikia madai yao na pia kuiomba Takukuru kuchunguza kwa kina kile walichokiita rushwa inayosambazwa na watu wa CCM.

Msimamizi wa Uchaguzi akiri barua
Kwa upande wake, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Protace Magayane amekiri kuwapo barua hiyo ya Chadema lakini akasema alikuwa nje ya ofisi hivyo asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa kina.

"Nimesikia kuwepo kwa barua hiyo lakini mimi nipo huku mkoani siwezi kuzungumzia chochote mpaka nirudi Igunga," alisema alipoulizwa kwa simu jana.


Nchemba abeza tuhuma
Akizungumzia tuhuma hizo, Nchemba ambaye pia ni Nbunge Iramba Magharibi, alisema madai hayo ya Chadema hayana ukweli wowote. Alisema kwamba alitoa Sh400,000 kwa wanakwaya kutoka katika jimbo lake na si Sh2 milioni i kama kinavyodai chama hicho.
“Ile kwaya ilikuwa imetokea jimboni kwangu na niliwapa Sh400,000, kila kwaya 200,000… hizo milioni mbili wanazosema sijui wamezitoa wapi labda walinitolea wao, mpigakura wangu hata nikutane naye wapi kama ana shida ninaweza kumsaidia fedha,” alisema Nchemba.
Alisema kauli ya kwamba ametoa baiskeli si ya kweli kwa kuwa chama hicho hakina mpango kama huo.
“Ila hawa wenzetu (Chadema) mbona wanalalamika wakati mambo bado kabisa, kama ni mpira hata mwamuzi (refa) hajapuliza kipenga, ila pamoja na yote hili jimbo ni letu,” alitamba Nchemba ambaye Meneja wa Kampeni za Uchaguzi wa Jimbo hilo.

Sau yanyooshea vidole vyombo vya habari
Chama cha Sauti ya Umma (Sau) kimelalamika na kuvinyooshea vidole vyombo vya habari kwamba havitendi haki katika kuripoti taarifa za uchaguzi wa Igunga kwa kile walichodai, vyombo hivyo vinatoa kipaumbele kwa baadhi ya vyama vichache.

Meneja wa kampeni wa Sau, Merkezedek Leseka alisema kumekuwapo na upendeleo wa wazi ambao unalenga kuvibeba vyama vya CCM, CUF na Chadema.

Leseka alisema chama chake kwa muda mfupi kimefanya maajabu Igunga lakini, wanahabari wanaoripoti habari za uchaguzi Igunga hawawapi nafasi licha ya baadhi kufika katika ofisi yao na kuchukua taarifa.

Alisema: "Jamani ndugu zangu wanahabari naomba mlichukue hili kama ni kilio cha Sau hamtendi haki kwetu mbona wengine mnawapa nafasi kubwa sana kwenye media (vyombo vya habari) zenu sisi hamfanyi hivyo?"

Alidai kwamba kumekuwapo na mkakati wa wazi wa kukipendelea Chadema huku akisema hakina nguvu kuzidi Sau na kutoa angalizo kwamba wanahabari wanaoandika habari za kukibeba chama hicho wataumbuka mwisho wa uchaguzi.

"Nawaambia sijui mtajificha wapi siku matokeo yakitangazwa maana Chadema tutawagaragaza mapema tu na hawana jipya wale,” alisema huku akisisitiza kuwa chama chake ndicho kitakachoibuka mshindi.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Mwikabe Mwita Waitara akizungumzia madai hayo ya Sau alidai kwamba chama hicho ni cha mfukoni na hakina hadhi ya kulumbana nao.Alidai chama hicho ni vibaraka wa CCM wanaotumika kukivuruga Chadema.

Ratiba ya Nec
Tayari Nec, imepanga Oktoba 2, mwaka huu kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa ubunge, Jimbo hilo la Igunga. Fomu za uteuzi wa wagombea wa vyama vyote zitatolewa kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 6, mwaka huu.

Kuanzia Septemba 6, itakuwa ni uteuzi wa wagombea ambao utaendelea hadi kesho yake, siku ambayo pia imepangwa kwa ajili ya kupokea pingamizi wakati kampeni zikitarajiwa kuanza Septemba 7 hadi Oktoba Mosi, mwaka huu na Oktoba 3 na 4 zitakuwa siku za kujumlisha matokeo na kutangaza mshindi.

No comments:

Post a Comment