Rais Jakaya Mrisho Kikwete
UTEUZI wa wakuu wapya wa mikoa uliotangazwa jana na Ikulu, umewagawa watu wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi na wanasiasa.Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili wameukubali na wengine waliuponda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walioponda uteuzi huo walisema hauna jipya kwa sababu hata hao walioondoka hawakuweza kutatua kero za wananchi.
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei, alisema haamini kama wateule hao wapya watakuwa na jipya na kwamba, uongozi wao hauwezi kuwa wa tija ikiwa Serikali haitabomoa mfumo wa utawala wake ambao alidai kuwa ni wa kifisadi.
“Huu uteuzi hauna jipya, wote ni wale wale tu kwani hata walioondoka hawakuweza kutatua kero za wananchi hawa walioingia nao wametoka katika mfumo uleule wa kifisadi,” alisema Mtei.
Mtei alieleza wasiwasi wake kuhusu utaratibu wa watu kupewa nyadhifa mbili akisema: “Ingawa katiba haikatazi, ni bora kipengele hicho kikafanyiwa marekebisho”.
"Hili sina tatizo sana kwa sababu ni jambo la kikatiba, lakini lazima tukubali kwamba, hapa kuna kasoro. Muhimu ni wananchi kuhakikisha wanapata katiba mpya inayotenganisha mambo hayo," alisema Mtei.
Kauli za wasomi
Dk Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kwamba, nafasi hizo hazina umuhimu, kwa sababu nchi imeweza kukaa muda mrefu bila kuwa na wakuu hao wa mikoa, lakini hakuna jambo lililoharibika.
Alisema, kutokana na hali hiyo, hakukuwa na umuhimu wa kuwateua wakuu wa mikoa kwa sababu ni ufujaji wa fedha za Serikali ambazo zingeweza kutumika kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
“Hivi vyeo havina umuhimu kwa sababu tumeweza kukaa muda mrefu bila kuwa na wakuu wa mikoa na wilaya na hakuna jambo lolote lililoharibika. Kwa hiyo uteuzi wao hauna maana kwa vile watendaji waliopo wanaweza kutimiza wajibu wao bila matatizo,” alisema Dk Mkumbo.
Alisema hali hiyo ni somo kwa Serikali kwamba, hakuna haja ya kuwachagua wakuu wa mikoa kwa sababu nchi inatumia gharama kubwa kuwahudumia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema uteuzi huo ni wa kichama zaidi kwani walioteuliwa wengi ni makada.
Hata hivyo aliwataka waliochaguliwa kuwa na moyo wa ushindani katika utendaji wao wa kazi ili kujiletea ufanisi uliokusudia na mwajiri wao ambaye ni rais.
“Uteuzi wa mwaka huu ni tofauti na miaka iliyopita ambao ulikuwa wa kijeshi zaidi kuliko wananchi wa kawaida. Mheshimiwa Rais kawateua makada ili kulinda maslahi ya chama chake,” alisema Dk Bana.
Wadau wengine
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi(Tucta), Nicolaus Mgaya, aliungana na Dk Kitila akisema kwa nafasi hizo kuwa wazi kwa muda mrefu ni dhahiri hazina umuhimu kwa maendeleo ya taifa.
Hata hivyo alisema walioteuliwa wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana kwa kasi katika mikoa yao.
“Kwa kweli serikali imeshindwa kuteua kwa wakati, hii inatokana na baadhi ya mikoa kukaa zaidi ya mwaka mmoja bila ya kuwa na viongozi, jambo linaloonyesha wazi kuwa, maendeleo ya mikoa hiyo inaweza kurudi nyuma,” alisema Mgaya.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa sheria, lakini kitendo cha rais kukaa muda mrefu bila kuwateua ni uthibitisho kwamba nafsi hizo hazina umuhimu.
Kadhalika Kibamba alikosoa uteuzi wa wabunge kuwa wakuu wa mikoa akiweka wazi kwamba viongozi hao hawawezi kutimiza wajibu wao wa kuwatetea wananchi wawapo bungeni.
“Mbunge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa hawezi kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wake, hawezi kuishughulikia serikali ikiwa imeshindwa kutimiza wajibu wake, kwa sababu yeye mwenyewe ni miongoni mwa watendaji wa serikali,” alisema Kibamba na kuongeza: “Wanapaswa kuteuliwa watu wengine ili waweze kushika nafasi hizo”.
Hata hivyo amepongeza hatua ya Rais kutambua umuhimu wa wanawake katika uteuzi huo ambao ni zaidi ya asilimia 30 na kwamba hiyo ni changamoto kwamba, wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa ufanisi.
Juzi, Rais Kikwete alitangaza wakuu wa mikoa 21 kati yao, 11 wamepandishwa vyeo kutoka kuwa wakuu wa wilaya na kwabadilisha vituo vya waliosalia katika nafasi hiyo ispokuwa, Perseko Ole Kone ambaye amebakia mkoa wa Singida.
Katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amewateua waliokuwa naibu waziri watatu ambao ni Mwantumu Mahiza, Ludovick Mwananzila na Joel Bendera, kuwa wakuu wapya wa mikoa.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa jijini Dar es Salaam iliwataja wakuu hao wa wilaya 11 waliopandishwa vyeo na mikoa yao kwenye mabano kuwa ni John Tupa (Mara), Saidi Mwambungu (Ruvuma), Chiku Gallawa (Tanga), Leonidas Gama (Kilimanjaro), Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma), Elaston Mbwillo (Manyara), Fabian Massawe ( Kagera), Fatma Mwassa (Tabora), Ali Rufunga (Lindi), Ernest Ndikillo (Mwanza) na Magesa Mulongo (Arusha).
Sehemu ya taarifa hiyo ilifafanua, "katika mabadiliko hayo, Rais aliwateua wakuu wa mikoa wapya 15, kuwabadilisha vituo vya kazi wakuu wa mikoa watano na wengine saba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu''.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakuu wa mikoa wengine wanne watapangiwa kazi nyingine na kuongeza kwamba wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye. |
No comments:
Post a Comment