Friday, December 9, 2011

Spika, Katibu wa Bunge wapingana posho

venance.chadema@yahoo.com

 Send to a friend
Thursday, 08 December 2011 21:04
Spika Anne Makinda

SAKATA la nyongeza ya posho za wabunge sasa limegeuka vita baina ya watendaji wakuu wa taasisi hiyo ya kutunga sheria; Spika Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashililah.

Hali hiyo inaonekana baada ya Dk Kashililah jana kuendelea kusisitiza kuwa kauli yake kwamba posho hizo hazijaanza kutolewa kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete hajasaini, bado ni sahihi na kuahidi kuweka mambo hadharani akirejea nchini kutoka jijini London.Dk Kashililah alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili akiwa London Uingereza kuhusu mgongano wa kauli na msimamo kuhusu posho hizo, uliojitokeza baina yake na Spika Makinda.

“Mimi ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Bunge. Na ninapozungumzia jambo nina uhakika na kile ninachokizungumza kwa kuwa najua wajibu wangu,”alisema Dk Kashililah.

Alisisitiza kuwa kauli aliyoitoa awali, inatokana na kile alichokuwa akikifahamu kwa mujibu wa mamlaka yake ya kiutendaji na madaraka aliyonayo kwenye ofisi hiyo ya Bunge.

Dk Kashililah alisema hana wasiwasi na kauli yake na hivyo akaomba apewe muda kwa kuwa wakati mwingine siyo vyema kuzungumzia jambo linalohusu ofisi akiwa nje ya nchi.

“Njoo ofisini (Jumatatu) nikisharudi  nitalielezea vizuri jambo hilo,” alisema alipotakiwa na gazeti hili kuelezea juu ya misimamo iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa dini, wasomi, wanaharakati na wanasiasa kumtaka ajiuzulu kutokana na kauli yake kuonekana kuwa ya uongo hasa baada ya Makinda kueleza kuwa posho hizo zimeshaanza kulipwa.

Dk Kashililah alisema anafahamu vyema wajibu wa mamlaka aliyonayo hivyo ataweka wazi ukweli wa mambo siku hiyo atakapoingia ofisini.Alifafanua kwamba anatarajia kurejea nchini wakati wowote mwishoni mwa wiki hii na Jumatatu atakuwa ofisini kwake Dodoma, tayari kutoa ufafanuzi huo.


Mgongano wa Spika, Kashilila
Mwishoni mwa wiki iliyopita Dk Kashililah alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kukanusha taarifa za uchunguzi zilizoandikwa na gazeti hili kuhusu ongezeko hilo la posho za kuhudhuria vikao vya Bunge.

Dk Kashilila alikiri kuwepo kwa mapendekezo hayo ya nyongeza za posho, lakini ofisi yake ilikuwa haina ruhusa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete kutekeleza mkakati huo.

Lakini tofauti na kauli hiyo ya Dk Kashililah, Spika Makinda alikiri nyongeza ya posho hiyo jijini Dar es Salaam katika mahojiano na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuzindua wa Ripoti ya Dunia ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki, idadi ya watu na vijana, Jumanne wiki hii.

Makinda alisema kwamba wabunge walianza kupata posho kiasi cha Sh200,000 kwenye vikao vya Bunge la Novemba mwaka huu.

Zitto awaka
Jana Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ambaye hata kabla ya nyongeza hiyo alikuwa mstari wa mbele kupinga posho za wabunge alisema ongezeko hilo ni batili kwa sababu halina baraka za Rais Kikwete.

“Spika wa Bunge anajua kwamba posho zote hulipwa baada ya Rais kuidhinisha,” alilalamika Zitto ambaye pia ni Naibu katibu Mkuu wa Chadema

Alisema posho alizotangaza Makinda hazikuidhinishwa  kwani uthibitsho wa kuidhinisha ni Masharti Mapya ya kazi kwa wabunge ambayo hayajatolewa na Ofisi ya Rais.”

Zitto ambaye alianzisha mgomo dhidi ya posho za wabunge, alisema kitendo cha kuanza kulipa posho mpya bila masharti mapya ya kazi za wabunge ni kukiuka sheria ya utawala wa Bunge kifungu cha 19.

Alisema kutokana na hali hiyo, Tume ya Bunge inapaswa kuwajibika kwa kutumia vibaya mamlaka yake.

Mbali na kuwajibishwa kwa Tume hiyo ya Bunge, Zitto alipendekeza posho mpya zifutwe na zilizolipwa zirejeshwe mara moja kwani zimelipwa kinyume na sheria.

“Spika anapaswa kuheshimu sheria ambazo Bunge limepitisha na kwenda kinyume na sheria kwa makusudi ni kosa la kuvuliwa Uspika,” alionya Zitto.

Wabunge wengine waliopinga nyongeza hiyo ni Januari Makamba wa Jimbo la Bumbuli,na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.


No comments:

Post a Comment